Tuesday, October 21, 2014

DAWA YA KUKAMATA WEZI WALIYOPEWA NA MGANGA WA KIENYEJI YAZUA BALAA TARIME

Watu saba kati ya 100 Kijiji cha Kenyamanyori, Kata ya Turwa, Wilaya ya Tarime walioshiriki kunywa dawa ya mganga wa kienyeji aliyeletwa kutoka Busia nchini Kenya wameingia kwenye wakati mgumu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya kulipa Sh3 milioni kila mmojaWanakijiji hao walikusanyika juzi asubuhi baada ya kengele ya kijiji kugongwa na uongozi, huku wakieleza kwamba ilikuwa siku ya nne kwa kengele hiyo kugongwa lengo likiwa ni kuzungumzia wizi unaoendeshwa na watu wasiojulikana.Inadaiwa wizi wa kuvunja maduka umekithiri kijijini hapo, baada ya wanakijiji hao kuwasili eneo la mikutano, walielezwa kusudio la kengele kuwa ilikuwa ni kutokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu.


Miongoni mwa waliovunjiwa duka ni Ayubu Wambura, anayedaiwa kuleta mganga kutoka Busia nchini Kenya kuwabaini wahusika, hivyo kila mmoja aliombwa kunywa dawa ya mganga huyo au kuacha maana ni hiyari.
Hata hivyo, walitahadharishwa kwamba kama aliyeshiriki hatakunywa dawa hiyo, itamuumbua maana aliyeibiwa atakuwa amekunywa.

Kabla ya kuanza kunyweshwa, mganga huyo aliomba wanakijiji iwapo kuna mhusika, ni vyema ajitokeze kabla ya kuingia gharama za kuwarejesha hali yao ya kawaida hazijaongezeka watakaponaswa.

Hata hivyo, wanakijiji walidharau wakidai ni mbabaishaji huyu hawezi lolote kwani hivyo ni vitisho.

Ilipotimu saa 5:00 asubuhi, mganga aliwaeleza ndani ya saa mbili tangu mtu anywe dawa yake atakuwa ameanza kuonyesha vitendo alivyokuwa akifanya wakati anaiba dukani.

Saa 6:00 mchana tayari dalili zilikuwa zimenza kuonekana kwa watu saba wakiwamo wafanyabiashara wenzake, pia yumo mwanamke wakiwa wamelewa wanafanya vioja, huku wengine wakila nyasi na kutafuna midomo.

Wambura alisema anachotaka ni kurejeshewa Sh12 milioni, zikiwamo gharama za mganga huyo, huku walionaswa na dawa hiyo wakitakiwa kulipa Sh3 milioni na kupewa siku tatu vinginevyo watageuzwa vichaa.

“Nimeibiwa sana ila ninavumilia, hii ni mara ya tano sasa, nimechoka na ninachotaka wanirudishie Sh12.5 milioni gharama niliyotumia ikiwamo mali zangu walizochukua, waliwahi kunivamia na mke wangu tunatoka dukani wakatukata mapanga hadi mke wangu akafa,” alisema Wambura.


Pia, tukio hilo lilishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Vanance Mwamengo, madaktari wa Hospitali ya Mji wa Tarime, madiwani na polisi na kwamba kutokana na wananchi kutokuchukua sheria mkononi, masuala hayo yatamalizwa kimila.