Peter Biaksangzuala amefariki akiwa hospitali Jumapili baada ya kuangukia kichwa chake aliporuka samasoti kushangilia bao aliloifungia Bethlehem Vengthlang FC - klabu yenye maskani yake Kaskazini Mashariki kwa jimbo la Mizoram.
Mchezaji huyo aliyekuwa ana umri wa miaka 23 alifunga bao hilo dakika ya 62 kuisawazishia timu yake dhidi ya Chanmari West FC Jumanne katika mchezo wa Ligi na akataka kushangilia kwa staili ya mfungaji bora wa kihistoria wa Kombe la Dunia, Miroslav Klose.
Biaksangzuala akikimbia kwenda kushangilia bao lake dhidi ya Chanmari West FC
Biaksangzuala alikosea katika kuruka kwake na akapigiza kichwa chini, kabla ya kupatiwa huduma ya kwanza uwanjani na kisha kutolewa nje kwa machela.
Biaksangzuala alikimbizwa katika hospitali ya Aizawl Civil ambako vipimo vya CT vilionyesha amepata madhara makubwa kwa undani na mara moja akahamishiwa chumba cha wagonjwa walio chini ya uangalizi maalum.
Chanzo kimesema: "Alijaribu kushangilia kama Mjerumani Klose, lakini akakosea kwa bahati mbaya. Alikaa hospitali kwa siku tano, lakini madaktari hawakufanikiwa kuokoa uhai wake,".
Taarifa nchini India zinasema kwamba Biaksangzuala alichangia macho yake wakati akiwa amelazwa hospitali.
Kwa ajili ya kumbukumbu ya kiungo huyo, Bethlehem Vengthlang FC imeamua kuipumzisha jezi namba 21 na Chama cha Soka Mizoram kimetoa taarifa katika Ukurasa wake maalum wa Facebook.