Tuesday, November 11, 2014

MWANAFUNZI ATESWA NA MACHO MIAKA 10

MTOTO Omar Mayunga (10) (pichani) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Sombetini jijini hapa, ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na ugonjwa wa kuvimba macho na anahitaji msaada wa kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro, Christian Medical Centre ‘KCMC’.
Mtoto Omar Mayunga akiwa na mama yake.
Mayunga anayeishi Sombetini na mama yake, alizaliwa na  ulemavu wa mdomo na macho bila kujulikana chanzo ambapo katikati ya mwaka huu alijitokeza mfadhili aliyemsaidia kufanyiwa upasuaji wa mdomo uliokuwa umechanika pande mbili kwa kujazwa nyama kisha kushonwa.
Akizungumzia ulemevu huo, mama mzazi wa mtoto huyo, Jafara Hussein ambaye ndiye anayezunguka naye mitaani kuomba msaada, alisema mwanaye alizaliwa akiwa  na ulemavu huo na kwamba hadi kufikia umri huo ameshindwa kumtibu  kutokana na kukosa fedha na muda wote macho huonekana kuvimba na kutiririka machozi.
Aliongeza kuwa, adha hiyo imesababisha kukimbiwa na mumewe, Mayunga Kondo ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo hali iliyomlazimu yeye kuacha shughuli zake za kuuza mbogamboga na kushinda akizunguka mtaani kuomba fedha kwa wasamaria wema waweze kumsaidia kupatikana kwa shilingi milioni 4 za matibabu ya upasuaji wa kuondoa uvimbe uliopo kwenye macho ya kijana wake.
“Hadi sasa sifahamu baba yake huyu mtoto alipo ila nasikia yupo Shinyanga. Alinikimbia na kunitelekeza mimi na wanangu wanne,’’ alisema mama huyo.
Alisema hadi sasa hajafanikiwa kupata kiasi hicho cha fedha kwani baadhi ya wasamaria wema wanaojitokeza wamekuwa wakitoa kiasi kidogo ambacho hujikuta akikitumia kwa ajili ya kuendesha familia yake kutokana na yeye kusimamisha biashara zake.
“Nalazimika kutembea na mgonjwa wangu kama unavyoniona ili jamii ishawishike kumchangia, muda mwingi nautumia kuomba kwenye mabaa na madukani kwa watu,” alisema mama Mayunga.
Mwanamke huyo aliomba kupitia habari hii, yeyote atakayeguswa na tatizo la mtoto wake anaweza kumchangia pesa kutumia namba 0766 350 664 ambayo ni yake.