Friday, December 26, 2014

DAKTARI ALIYETANDIKWA VIBOKO NA WANANCHI BAADA YA KUKUTWA BAA AMELEWA AVULIWA CHEO


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Magreth Nakainga amemvua madaraka Mganga Mkuu wa Zahanati ya Nyakabale, Josephat Msafiri kwa kukiuka miiko ya kazi yake na kulewa wakati wa kazi.

Mkurugenzi huyo aliamua kuchukua uamuzi huo juzi kutokana na tukio lililotokea Jumatano la daktari huyo kufunga kituo cha afya na kuacha wagonjwa wakiwa wamezidiwa, kisha kwenda kunywa pombe jambo lililowalazima kumchapa viboko akiwa baa.
 
“Tumeshamchukulia hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kumvua madaraka yake ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa Serikali,”alisema Nakainga.

Alisema kitendo alichokifanya kimeidhalilisha taaluma ya afya na madaktari kwa ujumla.

Alisema tabia kama hizo hazitavumilika kwa mtumishi yeyote atakayekiuka maadili ya kazi.


Pia alisema amepeleka wahudumu wa afya wakiwamo wauguzi wawili na daktari mmoja katika zahanati hiyo na huduma zinaendelea vizuri.