Tuesday, December 30, 2014

JIMBO LA KOROGWE; MTO UMEPITA JIMBONI, MAJI NI SHIDA

Mbunge wa Korogwe Nasir akichangia hoja ya mafuta bungeni.
Makala:Mwandishi Wetu,
BAADA ya wiki iliyopita safu hii kutembelea Jimbo la Temeke, wiki hii tupo Jimbo la Korogwe Mjini linaloongozwa na mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuph
Abdallah Nassir.
Baadhi ya wapiga kura waliozungumza na safu hii walisema matatizo mengi ya Jimbo la Korogwe yanatokana na usimamizi mbovu wa viongozi wa ngazi za juu.
Wapiga kura wa Kitongoji cha Kilole, wao walizungumzia shida ya maji kwamba ni tatizo sugu kwao ambapo wakati wa kampeni ya ubunge mwaka 2010, mheshimiwa Nassir aliahidi kutatua shida hiyo.
“Sisi hapa Kilole kama unavyoona, Mto Pangani unapita hapa lakini maji ni shida! Tuliamini mbunge wa sasa angetatua tatizo hilo lakini imekuwa sivyo na muda wa uchaguzi mwingine huo unakuja 2015,” alisema Kilaviani, mkazi wa Kilole-Misufini.
Mbunge anajibu: “Kusema ukweli suala la maji kwa Kitongoni cha Kilole limekwisha kwa sehemu kubwa, si kama ilivyokuwa wakati naingia madarakani. Sehemu ambazo bado, naamini mpaka mwakani katikati litakwisha kabisa.”
Wapiga kura wa Kitongoji cha Manundu (Makao Makuu ya Wilaya ya Korogwe) wao walilia na miundo mbinu, hasa barabara kama kutoka maeneo ya maungano ya  Barabara Kuu ya Korogwe Moshi na kwenda Hospitali ya Wilaya Magunga.
“Sisi tunaomba barabara zitengenezwe, hasa zile za kuingia mitaani, kama ile ya kutoka barabara kuu ya kwenda Moshi na kwenda Hospitali ya Magunga.“Lakini pia uwanja wa mpira Korogwe hakuna. Uliopo hauleti moyo wa kuinua michezo hapa Korogwe,” alisema Jumanne, mkazi wa Manundu.
Mbunge anajibu: “Barabara nyingine zimetengenezwa katika kipindi changu. Unajua si rahisi sana kukamilisha barabara zote za jimbo lakini ni mkakati ambao unaendelea mpaka barabara zote zitakapokuwa sawa.”
UCHAKAVU WA MJI
Baadhi ya wapiga kura walizungumzia namna Manispaa ya Korogwe ilivyochakaa na kutoa taswira mbaya kwa mji huo ambao ndiyo katikati ya Mkoa wa Tanga.
“Korogwe ya sasa inaonekana kuchakaa sana. Ni wilaya ipo katikati na zamani kulikuwa na minong’ono kwamba Korogwe ingekuwa mkoa lakini kwa mwendo wa sasa sidhani kama inawezekana.
“Mji unaonekana kuchakaa sana, umekuwa mwekundu kwa sababu barabara ni vumbi tupu. Hii inaonesha hata uchumi wa wilaya upo chini kwa sasa kuliko zamani.
“Kuna ujenzi wa stendi mpya kule Mbugani, umesimama hadi sasa hakuna kinachoendelea. Mimi nadhani ili kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye jimbo hili ni lazima kumpata mbunge mwenye nia ya dhati,” alisema Mwailengo, mkazi wa Manundu ambaye alisema yeye na Chadema ni damudamu.
Mbunge anajibu: “Wananchi wengine wanaamini hata ujenzi au ukarabati wa nyumba zao ni jukumu la mbunge. Nyumba anazosema zimechakaa ni za wananchi. Uchumi wa mtu mmojammoja unategemea namna familia ilivyo.
“Manundu ambayo ni makao makuu ya wilaya, nyumba nyingi ni za zamani, lakini watu kwa sasa wanajenga sana nje ya mji kama vile Majengo, Vetenari ambako viwanja vinapatikana kwa urahisi na wengi wamenunua kule.“Kuhusu stendi ni mkakati ambao unaendelea  na upo kwenye mpango wa mji, hakuna ubadhirifu au ufisadi kwenye ujenzi wa stendi hiyo.”
VITABU MASHULENI
Pia ni tatizo lililolalamikiwa sana na wapiga kura kwamba wanafunzi wanasoma katika uhaba wa vifaa vya kusomea.
“Mimi kama mpiga kura nadhani ninachoweza kukilalamikia ni vitabu mashuleni. Ni kilio cha muda mrefu sana,” alisema mama Musa, mkazi wa Majengo.Mbunge anajibu: “Wakati naingia madarakani suala la uhaba wa vifaa vya kufundishia lilikuwa sugu lakini kusema kweli nimepigania sana ambapo kama utatembea shule nyingi za jimbo langu watasema namna nilivyopambana.”
HUDUMA MBAYA HOSPITALI YA WILAYA
Wapiga kura wa Jimbo la Korogwe hawakuacha kuizungumzia Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga ambapo walisema:
“Hii hospitali yetu ya wilaya tatizo kubwa ni wauguzi. Unaweza kufika pale na mgonjwa wako ukakaa naye mapokezi kwa muda mrefu hata kama ana hali mbaya. Hii inawauma sana wananchi wa Korogwe.
“Mimi iliwahi kunitokea siku moja, tumempeleka mgonjwa pale matokeo yake akakaa mapokezi kwa muda mrefu, baadaye tukaoneshwa baiskeli ya kumpakia mgonjwa wetu hadi chumba cha matibabu tena kwa kumsukuma sisi wenyewe, ni haki kweli?” alihoji Dan Joseph, mkazi wa Kitongoji cha Kitonga.
Mbunge anajibu: “Hilo linawezekana kwani kila muuguzi anakuwa na wito tofauti na wengine. Nitalifuatilia hilo. Lakini kusema kweli mimi na viongozi wengine tumekuwa tukipigania sana kuhakikisha huduma kwenye hospitali tena kama ile ya wilaya inakuwa ya kujituma kwa wauguzi.”
NENO LA MWISHO
Mwisho, Mbunge Nassir alisema kuwa, ni vyema kama kuna ahadi hajaitekeleza wapiga kura wakamfuata yeye lakini ni mbaya sana watu kuendesha kampeni za chini kwa chini na kusema maneno ya kumpaka matope hali inayomshangaza.
“Kuna ahadi nimetekeleza zipo ambazo bado, nawaomba wapiga kura wangu tushirikiane jamani. Tabia ya watu kuanza kampeni za chini kwa chini si nzuri,” alisema.