Friday, January 2, 2015

2015 TUPUNGUZE SIASA, TUFANYE KAZI

Waziri mkuu Mizengo Pinda.
LEO ni siku ya pili tangu tumeanza mwaka 2015, ambao utakuwa na pilikapilika nyingi, pengine kuliko ilivyokuwa mwaka uliopita. Ni jambo la kushukuru Mungu kwamba tumefanikiwa kufika salama, kwa wale ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki, walio majeruhi na wagonjwa, tuwaombee kila dakika.
Tumeumaliza mwaka 2014 tukiwa na stress kubwa, maana mambo mengi ya kisiasa yalituachia makovu yasiyofutika, lakini pia kama taifa, tukirudi nyuma hatua kadhaa badala ya kusonga mbele. Tulikuwa watu wa blahblah nyingi karibu katika kila sekta.
Katika matukio makubwa, yote ni kama tulifeli, kwa sababu matarajio ya wananchi hayakuwa kama yalivyotokea, kiasi kwamba watu walizidi kupunguza imani kwa vyombo vya dola pamoja na watendaji wake, wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi wa Halmashauri na hata baadhi ya makamanda wa Polisi wa mikoa nchini.
Mathalan, katika hitimisho la rasimu ya pili ya Katiba Mpya, licha ya serikali kutumia fedha nyingi kuliwezesha Bunge Maalum la Katiba kufanya maboresho ya rasimu hiyo, kilichotokea kimewakatisha tamaa wananchi wengi. Licha ya ukweli kwamba Katiba inayopendekezwa ni halali kisheria, lakini katika nchi inayotaka demokrasia ya kweli, ingependeza zaidi kama ingekuwa ya maridhiano.
Hii ni kwa sababu kitendo cha wajumbe kutoka vyama vya upinzani kususia vikao hivyo, kwa madai kuwa vifungu vyake vilikuwa vinachakachuliwa na wenzao wa CCM, kumeifanya katiba hiyo kuonekana kama iliyotungwa na chama kimoja, jambo ambalo kama taifa, hatuwezi kujivunia.
Njoo kwenye sakata la fedha zilizochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Huku nako tumepiga siasa kiasi cha kujishangaza sisi wenyewe. Mamlaka zilizoteuliwa kihalali na Rais, kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zote zilithibitisha pasipo shaka kuwa hela zile ni za umma.
Na hata mhimili mwingine wa dola, Bunge nao ukakubaliana na vyombo hivyo na kutoa maazimio yaliyopaswa kutekelezwa na Rais ili kuhakikisha fedha hizo zinarudi na hatua za kisheria dhidi ya wahusika zinachukuliwa.
Lakini kwa mara nyingine, siasa za blahblah zimetembea kiasi cha kuwaduwaza hata wabunge wenyewe. Huu ni mzaha ambao kiukweli haupaswi kuruhusiwa kuendelea katika mwaka huu tuliouanza jana.
Tumefanya pia uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji  ambao umesimamiwa na serikali kwa maana ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Haukuwa katika kiwango cha kujivunia, vurugu nyingi zilitawala, polisi walitumia nguvu pasipo sababu, mauaji na hata dosari nyingi za makusudi zilizokuwa na malengo maalum.
Kwa ujumla, haukuwa uchaguzi huru, kwa sababu dosari nyingi zilizojitokeza, zilikuwa za kutengenezwa, ndiyo maana hata kufukuzwa kazi, kusimamishwa na kupewa onyo kwa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri, bado hakuwezi kuondoa lawama kwa watendaji wa serikali.
Yapo matukio mengine makubwa pia ya kitaifa yatatakiwa kufanywa mwaka huu. Ili tusonge, yatupasa kuacha blahblah, tufanye kazi. Panapotakiwa sheria, ifuatwe, tuache kupindisha maneno, tuache kulindana, kila mwenye majukumu ayatekeleze kikamilifu, anayezembea, ampishe Mtanzania mwingine kwa hiyari yake.