Monday, January 12, 2015

BINTI MIAKA 8 ABAKWA, AUAWA, ATUPWA!

Inauma sana! Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Ruanda Nzovwe jijini hapa, Elika Mkumbwa mwenye umri wa miaka 8 anadaiwa kubakwa, kuuawa na kutupwa kwenye jumba bovu (pagale) eneo la Mtaa wa Ilomba Village.
Makamanda wa Polisi wakiutoa mwili wa mtoto, Elika Mkumbwa kutoka kwenye  jumba bovu.
Akizungumzia tukio hilo lililojiri hivi karibuni, balozi wa mtaa huo, Ezekiel Mwakalundwa alisema kwamba alipata taarifa za kupatikana kwa mwili wa binti huyo majira ya saa 1:30 asubuhi kutoka kwa majirani waliokuwa karibu na eneo hilo.
Mapolisi wakiuchukua mwili huo kwa uchunguzi zaidi.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo aliongozana na majirani na baadhi ya ndugu wa marehemu hadi eneo ulipokutwa mwili huo na kushuhudia mwili wa mtoto  huyo ukiwa umelazwa ndani ya sinki la kuogea kwenye pagale hilo huku ukiwa hauna nguo.
Mwili wa mtoto, Elika Mkumbwa ukipakiwa kwenye gari la Polisi.
Mkumbwa alisema kwamba ulipopekuliwa mwili huo uligundulika kuwa mtoto huyo alifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kubakwa ambapo sehemu zake za siri zilikuwa zimeharibika vibaya na tayari mwili wake ulianza kuharibika.
Makamanda wa Polisi wakiondoka na mwili wa marehemu, Elika Mkumbwa.
Alisema alitoa taarifa polisi ambao walifika na kuchukua mwili wa binti huyo na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa upande wao majirani wanaoishi karibu na eneo hilo walidai kwamba tukio la kuuawa kwa mtoto huyo si la kwanza kwani matukio ya aina hiyo yamewahi kutokea zaidi ya mara tatu.
Mama mlezi wa mtoto huyo, Sara Mwandobo (katikati) akilia kwa uchungu.
Akizungumzia kwa masikitiko, mama mlezi wa mtoto huyo, Sara Mwandobo alisema binti yake alitoweka nyumbani tangu Januari 7, mwaka huu na kwamba aliaga anakwenda kufua nguo za shule lakini hakurejea.
Majirani wakishuhudia mkasa huo eneo la tukio.
Alisema baada ya kuona kimya alitoa taarifa kituo cha polisi ambao waliendelea kumtafuta binti huyo hadi mwili wake ulipopatikana ukiwa umeharibika.
“Inasikitisha sana. Huyu binti nilimchukua kwa mdogo wangu kijijini akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu,” alisema mama huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi hilo lipo kazini kuhakikisha mhusika anakamatwa na kufikishwa kwenye  mkono wa sheria huku mwili wa binti huyo ukiendelea kufanyiwa uchunguzi.