Sunday, January 4, 2015

MADHARA YA USAFIRI NA MISONGAMANO YA WATU VICHOCHEO VYA MAGONJWA

Ni wazi kuwa wengi wanatumia usafiri wa
umma kwa sababu ya uwezo, lakini unayo
madhara yake mengi kwa afya zao
Asubuhi inapofika, aghalabu asilimia 80 ya
Watanzania huongoza njia kutafuta usafiri


wa umma kwa ajili ya kuelekea katika
shughuli zao mbalimbali ambazo ni pamoja
na kujitafutia riziki.
Usafiri unaotumiwa zaidi ni wa mabasi ya
abiria, maarufu kwa majina mbalimbali hasa
daladala.
Hata hivyo, ndani ya daladala kuna kero
kubwa ya msongamano wa watu, ambao
haumpi abiria hata nafasi ya kupumua,
kupata hewa safi, kupiga chafya kwa
ustaarabu, kupenga au hata kukohoa.
Si hivyo tu kwani maeneo mengi nchini ni
yenye msongamano wa watu na ni makazi
yasiyopimwa. Hiki ndicho chanzo cha
kuenea kwa maradhi mengi kwa
Watanzania walio wengi.

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya Kifua
Kikuu Duniani, yaani Machi 24, imebainika
kuwa msongamano wa watu hasa kwenye
vyombo vya usafiri huenda kukawa ndicho
chanzo cha kuenea kwa maradhi hayo.
Hivi karibuni, Shirika la Afya Duniani (WHO)
lilitangaza kuwa watu milioni saba duniani
hufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa
hewa na nusu ya watu hao hufa kwa
sababu ya kuvuta hewa chafu kwenye
maeneo ya ndani yenye msongamano wa
watu.

"Ni lazima tupumue, na ndiyo maana ni
vigumu kuzuia maambukizi ya uchafuzi
huu," anasema mkurugenzi wa utafiti wa
mazingira wa Chuo cha Mazingira cha Kings,
Uingereza
WHO inaeleza kuwa, hewa chafu inayovutwa
kwenye mazingira husababisha vipande
vidogo vidogo kuingia kwenye mapafu na
kusababisha muwasho, na kudhurika moyo
jambo linalosababisha maradhi sugu ya
moyo au shinikizo la damu.

Kwa mwaka 2012, kulikuwa na vifo milioni
43 vilivyosababishwa na uchafuzi wa
mazingira wa ndani kwa ndani kama vile
msongamano wa watu, kupikia ndani kwa
kutumia kuni au mkaa.
Shirika hilo lilishauri kuwa ni vyema watu
wakaepuka kusafiri wakati wa
msongamano mkubwa, au kuepuka maeneo
yenye viwanda na kuacha tabia za kupika
ndani ya nyumba kwa mkaa au kuni.
Kwa mfano, msongamano unachangia
maradhi ya saratani wakati wa kuzaliwa,
kiharusi na maradhi ya moyo.

Utafiti uliofanywa na Robert Msigwa wa
Chuo Kikuu cha Dalian, China, kitengo cha
Sayansi ya Hesabu kuhusu madhara ya
usafiri wa umma Tanzania, ulibaini kuwa,
kwa kipindi cha miaka 12 (2000 hadi 2012)
Tanzania imezalisha tani 86,000 za hewa
chafu na kutokana na usafiri, msongamano
wa watu na magari yanayozalisha hewa
chafu. Uchafuzi huu husababisha maradhi
ya macho na mfumo wa hewa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya
mwili na ya Mfumo wa Hewa, Meshack
Shimwela anatolea mfano wa usafiri wa
daladala na kusema kuwa maradhi ya Kifua
Kikuu wakati mwingine husambaa kwa
sababu ya msongamano kwenye daladala.

"Iwapo madirisha yamefungwa ndani ya
basi la abiria, watu wamesongamana na
ndani kuna mgonjwa wa Kifua Kikuu
anayekohoa, hapo maambukizi huweza
kutokea," anasema.
Anasema hata hivyo iwapo mgonjwa wa TB
hajakohoa na madirisha ya gari yapo wazi,
hewa inaingia, basi hakuna maambukizi
yoyote yanayoweza kutokea.

Anaongeza kuwa, maradhi ya ngozi pia
huweza kusambazwa iwapo watu waliopo
kwenye msongamano wa basi la abiria
watakuwa wamegusana kwa kipindi fulani
na mtu asiye na maradhi kama hatanawa
kwa maji na sabuni baada ya muda mfupi.
Msongamano wa watu na magari
unasababisha maradhi ya ngozi, ajali,
zinaweza kutokea, msongamano watu
husababisha pia watu hao hutupa taka
hovyo jambo linalochochea kuenea kwa
maradhi.

Mtaalamu wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Frederick Mwanuzi
yeye analigusia suala hili katika pande mbili,
kwanza anasema msongamano wa watu
hasa ndani ya vyombo vya usafiri
husababisha kutokea kwa ajali
zinazosababisha vifo.

Pia, anaeleza kuwa, watu
wanaposongamana eneo moja ni rahisi
zaidi kuchafua mazingira kwa kutupa taka
hovyo ambazo nazo kwa upande mwingine
zinasababisha kuenea kwa maradhi.
"Lakini pia, maradhi ya mfumo wa hewa ni
rahisi kuambukizwa katika eneo lenye
msongamano wa watu, maradhi kama TB
husambaa kwa urahisi maeneo haya"
anasema Dk Mwanuzi.

Ripoti nyingi zinaeleza kuwa ongezeko la
idadi ya watu sambamba na lile la magari
yanayotumia mafuta kama ya dizeli na petrol
husababisha maradhi. Inaelezwa kuwa
kufuka kwa moshi wa magari, treni na
pikipiki zinazotumia mafuta hayo huchangia
uchafuzi wa mazingira ambao kwa kiasi
kikubwa husababisha maradhi ya mfumo
wa hewa kama pumu na mafua.

Wakati huo huo, Dk Innocent Godman,
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili na
Ushauri Nasaha kwa watumiaji wa dawa za
kulevya, yeye anaona athari kubwa zaidi
kwenye msongamano wa magari ambao
huwaathiri wanaadamu moja kwa moja.

Dk. Godman anasema msongamano wa
magari, husababisha uchafuzi wa mazingira
kwa kiasi kikubwa lakini pia husababisha
msongo wa mawazo kwa madereva na
abiria.
"Watu wanapokaa kwenye foleni kwa muda
mrefu, hupata msongo wa mawazo, ambao
husababisha hasira za kupoteza kipato na
kuchelewa kule wanakokwenda, hivyo
huweza kupata magonjwa ya akili,"anasema
Dk. Godman

Anasema, ndiyo maana si ajabu
kuwaona madereva na
makondakta wa usafiri wa umma
au hata magari ya watu binafsi,
wakitoleana lugha chafu hasa
kipindi cha msongamano mkubwa
wa magari.

"Maradhi yanayoingia moja kwa
moja mwilini mwa binadamu kwa
sababu ya msongamano wa watu
na magari ni maradhi ya mfumo
wa hewa, moshi wa kwenye
magari, msongamano ndani ya gari
husababisha watu kushindwa
kupata hewa safi na kuvuta hewa
yenye kemikali hatari," anasema.