Monday, January 5, 2015

PANYA ROAD WALISIMAMISHA JIJI, DAR SI SALAMA

Stori: Mwandishi Wetu
ACHENI jamani! Vurugu tuzisikie tu kwa wenzetu! Kitendo cha vijana wachache wasio na maadili wanaojiita Panya Road kufanya fujo kidogo katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar, wakazi wa jiji hilo wamekitafsiri kitendo hicho na kusema Dar sasa si sehemu salama tena ya kuishi, Ijumaa Wikienda lina ripoti kamili.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akionyesha picha ya baadhi ya wahalifu wa matukio ya uporaji.
Tukio hilo lililodumu kwa takriban saa nne na kusimamisha jiji, lilitokea usiku wa Ijumaa iliyopita ambapo awali, taarifa zilianza kusambaa kama moto wa kifuu kuanzia saa 12:00 jioni na kushika kasi zaidi majira ya saa 2:00 usiku, hali iliyosababisha wakazi wote wa Dar wakose amani kutokana na hali hiyo ya sintofahamu.
KILIVYONUKA IJUMAA
Siku hiyo, uvumi uliibuka kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter na Instagram kuwa vijana hao wameanzisha oparesheni maalum katika maeneo ya Magomeni-Kagera, Sinza, Tabata, Kijitonyama, Kimara, Mwananyamala, Kinondoni, Tegeta, Manzese, Ubungo, Kigogo, Tabata, Temeke, Gongo la Mboto na Buguruni na kusababisha taharuki kwa wakazi wake.
Sehemu ya jiji la Dar ikiwa tulivu kuhofia uhalifu wa 'Panya Road'.
MADUKA, BAA ZAFUNGWA
Kutokana na uvumi huo kukua kwa kasi, wafanyabiashara walifunga maduka yao mapema huku watu wakihamasishana kurudi majumbani na kutowasha taa kwa ajili ya usalama wao.
Akizungumzia tukio hilo, mkazi mmoja wa Legho, Ubungo jijini Dar, alisema mtaani kwao watu walizima taa kutokana na tahadhari hiyo huku kila  mmoja akimuomba Mungu, Panya Road wasiwafikie.
TUJIUNGE NAYE
“Nilikuwa natoka ‘home’ nawafuata washikaji zangu maeneo ya Sinza, Mapambano, hatua chache kutoka nyumbani nikakutana na kundi la watu wanarudi majumbani, wakasema Panya Road wanakuja turudi ndani na kuzima taa.
Baadhi ya wahalifu wa matukio ya uporaji.
“Pasipo kuhoji, nikarudi na kuzima kila kitu ndani hadi simu iliyokuwa ikitoa mwanga nikaiweka chini ya kochi,” alisema mkazi huyo wa Legho.
WANAUME WARUDI MAPEMA
Akizungumzia tukio hilo, mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Pendo, mkazi wa Sinza-Mori, Dar alisema licha ya tukio hilo kuzua taharuki kubwa, anamshukuru Mungu siku hiyo mumewe alirudi nyumbani mapema na kuwakumbatia wanaye jambo ambalo huwa halifanyi.
“Panya Road kwa upande mwingine wamesaidia jamani, nimekuwa nikimhimiza mume wangu kuwahi kurudi lakini leo (Ijumaa) amerudi mwenyewe mapema,” alisema Pendo.
Makamanda wa Polisi wakiimarisha ulinzi dhidi ya vitendo vya uporaji na unyang'anyi.
WATU WAKIMBIA HOVYO
Ijumaa Wikienda lilizungumza na wakazi mbalimbali wa jijini ambao walieleza namna ambavyo karibu kila kona watu walikuwa wakikimbia hovyo kwa kuibuka kwa taarifa kwamba Panya Road wako kwenye Bajaj wanakaribia maeneo yao.
“Tunatishana kweli, nilikuwa hapa Baa ya Kimboka, Buguruni watu wanasema Panya Road wanakuja, watu wamekimbia, wameacha simu zao, wengine wamekimbia bila kulipa bili, vurugu tupu lakini hatujawaona hao Panya Road,” alisema Ernest, mkazi wa Buguruni, Dar.
WAHUDUMU BAA WAGOMA KULIPWA, WALEVI WAACHA BIA MEZANI
Katika baa moja maarufu iliyopo Mlimani City, Dar ilishangaza kwani wakati wa mshikemshike huo wa Panya Road kwamba wanaelekea kuingia ndani, baadhi ya wahudumu waligoma kupoteza muda kwa kupokea fedha za bili badala yake walikuwa wakiwaomba wateja waondoke ili na wao wajiokoe.
Kama vile haitoshi, wateja walevi waliokuwa wameshaanza ‘kuwaka’ kwa bia za wikiendi, waliacha vinywaji vyao juu ya meza na kutimua kuwaogopa hao Panya Road ambapo habari zilisikika kuwa wana mapanga, visu na wapo pia wenye bunduki.
Raia wakishuhudia ulinzi ukiimarishwa na makamanda wa Polisi.
KAMANDA APASUA JIPU
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alizungumza na wananchi usiku huohuo laivu kupitia Televisheni ya Taifa, TBC1 na ITV na kufafanua ukweli kuhusiana na kundi hilo.
“Tumepata taarifa za kundi hilo (Panya Road) inasemekana kuwa kundi la wahalifu hao lina tabia ya kulipiza kisasi. Aaa! Jana (Alhamisi) kuna mwenzao mmoja anadaiwa aliuawa na wananchi wenye hasira kali sasa baada ya kumzika mwenzao (Mohamed Ayub) maeneo ya Kihatu Kagera Mikoroshini (Dar), waliahidi kulipiza kisasi.
“Tulipata taarifa hizo mapema, vijana wetu wakaenda mpaka makaburini na kufanikiwa kukamata vijana wawili.
“Ile milio ya mabomu ni polisi walilazimika kutumia silaha hizo ili kuwatawanya vijana wengine. Tumetuma difenda za kutosha kila sehemu,” alisema Kamanda Kova huku akiwataka wananchi kuwa na amani kwani polisi wametawanywa kila kona ya jiji ili kuwalinda.
POLISI WAPONGEZWA
Wakati hofu ya Panya Road ikituliatulia, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar wamelipongeza jeshi la polisi kwa jinsi walivyopambana na vijana hao ili kurejesha amani na kuhakikisha ulinzi unakuwepo.
“Tunalishukuru sana jeshi la polisi, hawakuchelewa, ndani ya muda mfupi walikuwa wapo kila mahali wakilinda usalama,” alisema John, mkazi wa Tandale.
PANYA ROAD NI NINI?
Panya Road ni kundi lililoibuka miaka miwili iliyopita ambapo linawahusisha vijana wasio na kazi katika Jiji la Dar ambao hujikusanya mitaani na kuwashurutisha watu kwa silaha za jadi kusalimisha mali zao kwao.
Mbali na Panya Road, makundi mengine ambayo ni tishio jijini Dar ni Mbwa Mwitu na Watoto wa Mbwa. Kuna wakati wananchi waliamua kuchukua jukumu la kuwachoma moto hadharani vijana hao pale wanapokamatwa katika uhalifu, kwa mbali walipotea, huenda sasa wamerejea.
WANAZURURA MCHANA NA USIKU
Imeelezwa kuwa, kazi hiyo ya uporaji wamekuwa wakiifanya mchana na wakati mwingine usiku pasipo kuwa na hofu ya kutiwa nguvuni na Jeshi la Polisi Tanzania.
PANYA ROAD 36 WATIWA NGUVUNI
Baada ya siku ya tukio kupita, kesho yake, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa rasmi kuhusu matukio hayo na kueleza kwamba tayari vijana 36 walikuwa wakishikiliwa na jeshi hilo na kwamba taratibu za kipolisi zilikuwa zinaendelea ili kuwafikisha watuhumiwa wote mahakamani.
ULINZI NI JUKUMU LA KILA MTU
Vikundi hivi vinavyoibuka na kufanya vurugu mitaani ni vijana wetu ambao tunawafahamu hivyo ni vyema wananchi tukashirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha tunawakamata na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria ili kulinda amani-Mhariri.