Watu watano wamefariki dunia akiwemo dereva wake baada ya gari waliyokuwa wamepanda aina ya Noah kupasuka tairi la nyuma na kuacha njia hivyo kusababisha vifo vya watu hao katika eneo la Fukayosi katika Tarafa ya msata wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha gari namba T 252 DCB aina ya Toyota Noah lililokuwa likiendeshwa na Ramadhana Masapala (32) lilikuwa likitokea kwenye kituo cha afya cha Miono kuelekea hospitali ya wilaya ya Bagamoyo.
Kamanda Matei alisema kuwa ndani ya gari hiyo alikuwepo mama mjamzito aliyekuwa akipelekwa hospitali Shukuru Jaba (30) na muuguzi wa kituo cha afya cha Miono Mariamu Omary ambao wao walijeruhiwa.
Alisema wote waliofariki dunia walikuwa ni wakazi na wakulima wa Miono na kuwa miili ya marehemu hao imepelekwa hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo huku majeruhi wawili wakipelekwa kituo cha afya cha Miono huku mama mjamzito akiandaliwa kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Via>>ITV