Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Segerea, akisindikizwa na askari baada ya kuhudhuria kuapishwa kwa wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa wa Jimbo hilo jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni baadhi ya wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani, wakishinikiza kutolewa kwa Dk. Mahanga.
Vurugu katika zoezi la kuapisha wenyeviti wateule wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji zimepamba moto, ambazo zimesababisha Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, kujikuta akizomewa na wananchi na kusababisha zoezi hilo katika baadhi ya mitaa na vitongoji katika maeneo mbalimbali nchini kukwama.
Dk. Mahanga, ambaye pia ni Mbunge wa Segerea (CCM) alikumbwa na masaibu hayo wakati wa hafla ya kuapisha wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa katika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam na hivyo, kulazimika kuondolewa katika ukumbi wa Halmshauri ya Manispaa ya Ilala wa Anartoglou chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Kabla ya kukumbwa na mkasa huo, Dk. Mahanga alifika katika ukumbi huo ili kushuhudia kuapishwa kwa viongozi wa serikali za mitaa wanaotoka katika jimbo lake.
Katika eneo hilo, kulikuwako na mchanganyiko wa watu, wakiwamo wapambe waliokuwa wakishuhudia zoezi hilo.
Kitendo cha kumzomea Dk. Mahanga kilifanywa na wananchi hao waliokuwa wamesimama mlangoni katika ukumbi huo uliokuwa ukitumika kuapishwa viongozi hao.
Kutokana na mchanganyiko huo wa watu, haikuwa rahisi kufahamu waliomzomea Dk. Mahanga wanatoka chama gani cha siasa.
Tukio hilo lilianza muda mfupi baada ya kuingia zamu ya kuapishwa wenyeviti na wajumbe wa jimbo la Segerea baada ya zoezi hilo kumalizika kwa viongozi wanaotoka katika majimbo ya Ukonga na Ilala.
Wakati akitoka, alipofika mlangoni, umati wa watu waliofurika katika ukumbi huo, walianza kumzomea, huku wakimuita “mwizi” bila kufafanua alichoiba.
Watu hao waliendelea kufanya hivyo hadi Dk. Mahanga alipoondoka katika eneo hilo, huku akisindikizwa na askari polisi kupanda kwenye gari lake.
Awali, kabla ya kuanza kuitwa majina ya wenyeviti na wajumbe wanaotoka katika mitaa iliyoko Jimbo la Segerea kuingia katika ukumbi kwa ajili ya kuapishwa, Dk. Mahanga alikuwa tayari ameingia ukumbini humo ili kusubiri kushuhudia zoezi hilo.
Hata hivyo, watu hao walipomuona, walianza kupiga kelele wakimtaka aondoke.
“Tunamtaka Dk. Mahanga aondoke. Ameingia kufanya nini humo ukumbini wakati hahusiki?” walisikika baadhi ya watu wakihoji.
Wakati huo wajumbe na wenyeviti hao wateule kutoka mitaa iliyoko katika jimbo hilo wakiwa nje kusubiri kuitwa majina ili kuingia ndani ya ukumbi wakaapishwe.
DK. MAHANGA ANENA
Akihojiwa na waandishi wa habari juu ya kumtaka aondoke, Dk. Mahanga alisema yeye kama mbunge wa jimbo hilo, alienda kushuhudia viongozi wake wanavyoapishwa, hivyo asingeondoka.
Hata hivyo, alisema baada ya dakika chache, aliamua kuondoka na ndipo alikumbwa na zomeazomea hiyo na kuitwa “mwizi”.
“Mimi Kama Mbunge wa Segerea, nimekuja kushuhudia wenyeviti na wajumbe wangu kutoka mitaa 59 wanavyoapishwa, hivyo siwezi kuondoka,” alisema Dk. Mahanga.
ULINZI WAIMARISHWA
Zoezi hilo katika majimbo matatu ya Wilaya ya Ilala; ya Ilala, Ukonga na Segerea, lilianza saa 2.00 asubuhi, huku likiwa limetawaliwa na ulinzi mkali wa askari polisi waliokuwa wamezagaa ndani na nje ya ukumbi.
Ulinzi uliimarishwa kufuatia kutokea kwa vurugu juzi katika Wilaya ya Kinondoni na kusababisha Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi kutuliza ghasia zilizozuka wakati wa uwa zoezi hilo lililofanyika kwa viongozi wa serikali za mitaa iliyoko wilayani humo.
KASORO ZILIZOJITOKEZA
Pamoja na zoezi hilo kuanza vizuri katika katika Jimbo la Ilala, kasoro zilianza kuonekana walipoanza kuapishwa viongozi wa Jimbo la Ukonga.
Hali hiyo ilitokea baada ya kutokea mkanganyiko katika Mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’, ambako walijitokeza viongozi wawili wa nafasi ya mwenyekiti, huku kila mmoja akidai kuwa ndiye mshindi halali.
Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala, ambaye ndiye kiongozi wa zoezi hilo, Mashauri Musimu, alipotaka mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo kusimama, walisimama wawili mmoja akiwa ni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mwingine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kuona hivyo, wapambe wa mgombea wa Chadema waliokuwa wameingia ukumbini, walisimama na kuanza kupiga kelele wakimtaka mgombea wa CCM kuondoka wakidai hakushinda.
Hali hiyo ilizua taflani kubwa, ambayo hata hivyo, ilizimwa baada ya mwanasheria huyo kusema anauacha kiporo mtaa huo hadi hapo utata huo utakapopatiwa ufumbuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari, aliyekuwa mgombea wa Chadema katika mtaa huo, Patricia Mwamakula, alisema uchaguzi katika mtaa wao ulifanyika vizuri, lakini matokeo hayakutangazwa.
Mwamakula alisema hali hiyo ilitokana na kura kuchomwa moto na watu aliodai kuwa ni wafuasi wa CCM baada ya kugundua kuwa wameshindwa.
Alisema pamoja na kutangaziwa kuwa uchaguzi huo ungerudiwa Desemba 21, mwaka jana, walishangaa baadaye kuona matokeo yakibandikwa kinyemela, huku yakionyesha kuwa CCM ndiyo iliyoshinda.
Mwamakula alidai hilo lilifanyika kwa kuwa CCM tangu mwanzo walikuwa wameapa kuwa hawawezi kukubali mtaa huo kuchukuliwa na upinzani kwa kuwa anaishi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Mgombea wa CCM, Omari Mkali, alisema yuko tayari kusubiri maamuzi yoyote yatakayofikiwa dhidi ya utata uliopo katika mtaa huo.
Mtaa mwingine uliotokea utata ni wa Migombani, ambao nao matokeo yake hayakutangazwa, lakini kinyemela yakabandikwa kinyemela na kuonyesha mgombea wa CCM ameshinda na hivyo, kuzua kelele.
Kelele hizo zilizuka wakati jina la mshindi huyo lilipoitwa kwa ajili ya kuapishwa na hivyo, kuzua mvutano baina ya wafuasi wa CCM na wale wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa); vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi, ambao walitaka aliyekuwa mgombea wao ndiye aapishwe kwa madai kwamba, ndiye aliyeshinda.
Mtaa mwingine uliozua utata ni wa Guruka kwa Kalala ulioko katika jimbo la Ukonga, ambao baadhi ya majina ya wajumbe wa CCM walioshindwa yalionekana katika orodha ya washindi, lakini ya wajumbe watatu wa Ukawa, ambao ndiyo wanaodaiwa kuwa washindi halali hayakuonekana.
Hali hiyo ilimlazimu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Dorkasi Lukiko, kuanza kulalamika kwa kusema hawatambui wajumbe hao.
Alisema katika mtaa wake, washindi wawili wa nafasi ya ujumbe walitoka CCM na watatu Ukawa, lakini walikuta majina ya wajumbe wa Ukawa yametolewa na kuwekwa ya wa CCM ambao hawakushinda, akiwamo aliyekuwa akipambana naye katika nafasi ya uenyekiti.
Pamoja na majina ya wajumbe wa CCM waliodaiwa siyo washindi kuwapo katika orodha ya majina ya washindi, hawakufika katika eneo hilo kwa ajili ya kuapishwa.
Hata hivyo, kiongozi wa zoezi hilo alitatua tatizo hilo na kutangaza majina ya wajumbe wa Ukawa kuwa ndiyo walikuwa washindi na ndiyo walioapishwa.
Mwanasheria huyo alitangaza kwamba hataweza kuapisha wenyeviti na wajumbe kutoka mitaa ya Kigogo Fresh ‘B’, Migombani, Misewe, Machimbo hadi hapo kasoro zilizojitokeza zitakapotatuliwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mgeule (CCM), Kata ya Buyuni, Mariki Shemtandula, aliwataka viongozi hao kusimamia majukumu yao kwa kutatua changamoto na siyo kutumia fursa waliyoipata kwa maslahi yao binafsi.
BUNDA UAPISHAJI WAKWAMA
Wakati hayo yakijiri jijini Dar es Salaam, pia uapishaji wenyeviti wa vitongoji wa mamlaka ya mji mdogo wa Bunda, mkoani Mara, jana liliingia dosari baada ya kujitokeza wagombea wa vyama vya CCM na Chadema wakitaka waapishwe kwa madai kuwa wote ni washindi.
Zoezi hilo pia liliingia dosari baada ya wagombea wa viti maalumu kupitia Chadema, kujitokeza 10 badala ya watano.
Baadhi yao walidai kuwa majina yao ndiyo yalipendekezwa, lakini sasa yameingizwa ya wanawake, ambao ni ndugu wa viongozi hao.
Kufuatia hali hiyo, mwanasheria wa halmashauri hiyo alitoa muda siku mbili kumaliza mgogoro huo ili wapeleke majina yanayostahili.
Vilevile, zoezi hilo liliingia dosari, baada ya mwanasheria wa halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Philpo Shoni, kuwaita wenyeviti wa vitongoji vya Kabarimu na Nyasura B, ili waapishwe na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Safina Simufukwe, na ndipo wakajitokeza wagombea wa vyama vyote viwili.
Waliojitokeza kuwa ndiyo waliochaguliwa katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa katika Kitongoji cha Kabarimu, ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bunda (CCM), Pastory Ncheye na mgombea wa Chadema, Jackob Sospeter Maiga.
Katika Kitongoji cha Nyasura B, alijitokeza Julius Magambo Wassira wa Chadema na Sasta Mkama wa CCM, ambao kila mmoja anadai kuwa ndiye anayepaswa kuapishwa kwa sababu ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, mwanasheria wa halmashauri hiyo alipatwa na wakati mgumu kufafanua kwamba, majina ya washindi aliyonayo ni ya wagombea wa CCM.
Jambo hilo lilipingwa vikali na wagombea wa Chadema pamoja na wafuasi wao kwamba, uchaguzi katika vitongoji hivyo ulivurugika na kwamba, walitangaziwa kwamba utarudiwa Desemba 21, mwaka jana, lakini haukurudiwa.
Kufuatia hali hiyo, mwanasheria huyo alitangaza kuwa zoezi hilo limesitishwa mpaka hapo watakaopewa utaratibu mwingine.
Kauli hiyo ilipokelewa na wagombea wa Chadema kwamba, ametenda haki, kwani bila hivyo, ungetokea uvunjifu wa amani kwa kuapisha mgombea, ambaye hakutangazwa na msimamizi wa uchaguzi.
Hata hivyo, wagombea wa CCM katika vitongoji hivyo, Ncheye na Sasta walidai kuwa katika uchaguzi huo, walishinda kihalali, kwani wasimamizi wa uchaguzi walitangaza majina yao kwamba, ni washindi.
Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Safina Simufukwe, aliendesha zoezi la kuapisha wenyeviti wa vijiji, vitongoji na wajumbe wa serikali za vijiji kutoka katika kata mbalimbali za wilaya hiyo kwa amani na utulivu.
SABA BADO WASHIKILIWA DAR
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, lilisema jana kuwa bado linawashikilia watuhumiwa saba wa tukio la vurugu za kuapishwa kwa wenyeviti wa mitaa, lililotokea juzi. Lililotokea katika manispaa ya Kinondoni.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Camilius Wambura, alisema watuhumiwa hao bado wanaendelea kushikiliwa ili kukamilisha taratibu za upelelezi.
“Bado tunaendelea kuwashikilia watu saba, ambao walihusika katika vurugu zilizofanyika jana (juzi) katika zoezi la kuwaapisha wenyeviti wa mitaa. Ndani ya siku mbili hizi upelelezi utakuwa umeshakamilika na hatua nyingine zitafuata,” alisema Kamanda Wambura.
Alisema waliokamatwa walibainika kufanya vurugu za kuwapiga na kuwajeruhi watu wengine.
Juzi jeshi hilo lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa vyama vya upinzani waliokuwa wakizuia kuapishwa kwa wenyeviti wa mitaa waliochaguliwa Desemba, mwaka jana kwa madai kuwa hawakushinda kihalali.
Imeandikwa na Ahmed Makongo, Bunda, Mary Geofrey, Leonce Zimbandu na Elizabeth Zaya, Dar.