Monday, January 5, 2015

WIZARA YATOA MITAALA MIPYA YA UALIMU..STASHAHADA MIAKA MITATU BADALA YA MIWILI

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa mitaala mipya na idadi ya vyuo vilivyoruhusiwa kutumia mitaala hiyo ambayo wanafunzi wa ualimu wa ngazi ya Stashahada watasoma kwa miaka mitatu tofauti na ilivyozoeleka kusoma miaka miwili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa kwenye mtandao wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), na kusainiwa na Katibu Mtendaji wa Nacte, Dk. Primus Nkwera, alisema vyuo 46 ndivyo nyenye sifa ya kutoa mafunzo hayo.

Mitaala hiyo imeanza kutumika kwa mwaka wa masomo 2014/15 na kwamba iliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake za Nacte, Taasisi ya Elimu (TIE) na Baraza la mitihani ya Taifa (Necta).

Dk. Nkwera alisema mitaala hiyo ni kwa masomo ya ualimu ngazi ya diploma ya kawaida (NTA level 6) na Diploma ya juu (NTA Level 7), ambayo inakusudia kumwezesha mhitimu kukuza uwezo wake kwa kitaaluma katika masomo ya elimu ya msingi na sekondari na masuala mtambuka ili aweze kudhihirisha uelewa mkubwa kwenye masomo anayofundishwa katika ngazi hizo za elimu.

Aliitaja mitaala iliyoidhinishwa ni propgramu za stashahada ya kawaida ya elimu ya awali na msingi na stashahada ya juu ya elimu ya sekondari kwa miaka mitatu 

“Kwa walimu wenye cheti (daraja A), watasoma stashahada ya elimu ya msingi kwa muda wa miaka miwili ngazi ya tano na sita…kwa kuwa mitaala ni mipya na propgramu za mafunzo ni mpya, kuna baadhi ya vyuo vya ualimu na idara za elimu za baadhi ya vyuo vikuu viliteuliwa kutoa mafunzo haya kwa mwaka 2014/15,” alifafanua.

Katibu huyo alisema chuo chochote ambacho hakimo katika orodha ya Nacte hakitaruhusiwa kutoa mafunzo ya ualimu ngazi ya stashahada kwa kutumia mitaala mipya na kwamba utaratibu unaandaliwa wa kuongeza idadi ya vyuo vitakavyotoa mafunzo hayo kwa mwaka wa masomo 2015/16 iwapo vitakidhi vigezo vilivyowekwa.

Chini ya mitaala mipya kuanzia sasa hakutakuwa na walimu wa ngazi ya cheti au astashahada ambao waliandaliwa kwa ajili ya kufundisha shule za awali na msingi huku wa ngazi ya stashahada wakiandaliwa kwa ajili ya kufundisha sekondari.

Kwa utaratibu mpya shule za msingi walimu watakaofundisha ni wenye elimu ya diploma ya kawaida na sekondari ni wenye diploma ya juu na shahada.