WATOTO wa bondia bingwa wa dunia anayetambuliwa na shirikisho la WBE, Francis Cheka aliye gerezani, wamemliza babu yao, Boniface Cheka ambaye ni baba mzazi wa mwanamasumbwi huyo wakati alipowatembelea nyumbani kwao, kwa mara ya kwanza tangu kutolewa kwa hukumu hiyo wiki mbili zilizopita.
Mzee huyo ambaye makazi yake yako Dar es Salaam alifika mjini hapa kwa mara ya kwanza tangu mwanaye ahukumiwe, akiwa ameongozana na ujumbe kutoka Shirikisho la Ngumi la TPBO chini ya Rais wake, Abdalah Ustaadh.
Ujumbe huo ulifika mjini hapa Jumapili iliyopita na kwenda moja kwa moja katika gereza la Manispaa alikofungwa bondia huyo, ambako baada ya kumsalimia, walikwenda nyumbani kwake, ambapo baada ya kuwaona watoto na mkewe, mzee huyo naye alijikuta akishindwa kujizuia na hivyo kuangua kilio.
Awali wakiwa gerezani hapo, msafara huo ulishuhudia umati mkubwa wa mashabiki waliofika kwa ajili ya kumuona bondia huyo kipenzi chao, aliyefungwa kwa kosa la kumpiga ngumi meneja wa baa yake. Hata hivyo, wengi wa watu hao walikataliwa kumuona.
Rais wa TPBO, Ustaadh, alisema walikuja mjini hapa wakiwa na mwanasheria wao, ambaye amewaambia kuwa watalazimika kwanza kufika mahakamani ili kujua hatua za kuchukua, katika harakati za kutaka kumtoa hatiani, bondia huyo aliyekuwa kipenzi cha wengi.