Friday, February 6, 2015

CCM YABOMOA JENGO LA TANU JIJINI DAR ES SALAAM

Wananchi wakiangalia jengo la ofisi ndogo
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) la
Lumumba, ambapo kilizaliwa chama cha
Tanu lililobomolewa kupisha ujenzi wa jengo
jipya la chama hicho Dar es Salaam jana
JENGO la ofisi ndogo la Chama Cha
Mapinduzi (CCM) katika Mtaa wa
Lumumba Dar es Salaam ambako ndiko
kilizaliwa Chama cha Tanu limebomolewa
ili kupisha ujenzi wa jengo jipya la chama
hicho.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema jengo hilo limebomolewa
kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.
"Tunachokifanya katika jengo hili ni
ukarabati wa kawaida,"alisema Nape
wakati akielezea jengo hilo ambalo
limebomolewa jana kwa kutumia
tingatinga.
Kutokana na kubolewa kwa jengo hilo ,
viongozi wa ngazi mbalimbali akiwemo
Katibu Mkuu wa CCM,Abdulrhaman
Kinana , watakuwa katika Jengo la Umoja
wa Vijana wa chama lililopo barabara ya
Morogoro, wakati ukarabati wa jengo hilo
lililobomolewa ukiendelea.
Awali baadhi ya makada wa chama hicho
waliokuwa eneo hilo, walidai kuwa jengo
hilo la Tanu limebolewa ili kupisha ujenzi
wa jengo la kisasa ambalo litatumika kwa
ajili ya kitega uchumi.
Makada hao walisema jengo hilo
litakapokamilika litakuwa la kisasa zaidi
tofauti na jengo ambalo lilikuwepo eneo
hilo.