Wednesday, February 4, 2015

CHEKA ALIVYOHENYESHWA MAHAKAMANI

BONDIA bingwa wa dunia wa WBF uzani wa Kati, Francis Cheka ambaye juzi alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kumpiga mtu ngumi, alihenyeshwa kiasi cha kutosha kabla ya kupandishwa kwenye karandinga la Magereza lililompeleka kuanza maisha mapya katika gereza la Manispaa ya mkoa.
Awali, baada ya hukumu hiyo, Cheka alipelekwa katika chumba ambacho mahabusu hukaa kusubiri kuondoka na akiwa huko, alionekana akikabidhi baadhi ya vitu alivyokuwa navyo kwa ndugu na jamaa zake.
Bondia bingwa wa dunia wa WBF uzani wa Kati, Francis Cheka akiwa chini ya ulinzi mkali.
Wakati akiondolewa kwenda kupanda gari, Cheka alichukua simu yake na kuwapigia baadhi ya marafiki zake kuwajulisha juu ya msala huo, lakini Polisi hawakumruhusu kuendelea na jambo hilo, kwani walimnyang’anya na kumpeleka garini, ambako aliungana na mahabusu pamoja na wafungwa wengine.
Bondia Cheka akinyang'anywa simu asiendelee kuongea na marafiki zake.
Baadhi ya ndugu na jamaa wa Cheka waliokuwepo mahakamani hapo, waliangua kilio baada ya hukumu hiyo, akiwemo mkewe ambaye inasemekana kuwa ni mgonjwa. Mdogo wake naye aliangua kilio kikubwa kiasi cha kusaidiwa na meneja wa bondia huyo.
Cheka akichukuliwa na mahabusu wengine kwenye karandinga kwenda kuswekwa lupango.
Wakizungumzia hukumu hiyo, baadhi ya wakazi wa mjini hapa walisema Cheka aliichukulia kirahisi kesi hiyo na ndiyo maana amehukumiwa, kwani tokea kuanza kwake, hakuwahi kupeleka shahidi na hata siku ya hukumu, alishindwa kutoa utetezi wowote.