Friday, February 6, 2015

LUNGI: NIMEFANYA SANA BIASHARA YA KUUZA UNGA

Wiki hii katika kolamu yetu hii tunaye Lungi Maulanga, msanii wa filamu Bongo ambaye pia anafanya biashara. Mwandishi Wetu Hamida Hassan alikutana naye maeneo f’lani jijini Dar na kumbana kwa maswali 10 ambayo aliyajibu kwa umakini wa hali ya juu. Tiririka naye…
Mwigizaji wa Bongo Muvi, Lungi Maulanga.
 Ijumaa: Hebu tuambie kuhusu maisha yako ya kimapenzi.
Lungi: Nina mpenzi wangu ambaye nampenda sana na naamini bila yeye maisha yangu hayajakamilika.
 Ijumaa: Hivi siku ukimfuma huyo mpenzi wako na mwanamke mwingine utajisikiaje na utachukua hatua gani?
Lungi: Kimsingi nitaumia sana lakini sitakuwa na jinsi itabidi nimuache maana sipendi kusalitiwa.
Ijumaa: Mastaa mnatisha kwa kuchuna mabwana, wewe vipi ulishawahi kupitia maisha hayo ya kuchuna mabuzi?
Lungi: Nimeshawachuna sana kwani wamekuwa wakinifuata wao, si unajua nilivyo mrembo na shepu ninayo ndiyo wanachanganyikiwa kabisa.
Ijumaa: Kwa hiyo umeshatembea na wanaume wengi kwa sababu ya pesa, si ndiyo?
Lungi: Mimi mjanja bwana, wengine naishia kuwachuna tu lakini hawaoni ndani.
Ijumaa: Hivi mtu akikuuliza ni kazi gani inakuweka mjini utamjibuje? Maana unaonekana upoupo tu.
Lungi: Mimi ni mfanyabiashara, huwa nakwenda Sauzi, China na Dubai kwa ajili ya kuleta nguo na vitu vya wanawake.
Ijumaa: Wafanyabiashara wengi hasa wanaokwenda nchi hizo ulizotaja wanadaiwa kufanya biashara ya ‘sembe’. Wewe ushawahi kubeba mzigo?
Lungi: Ukweli nimewahi kubeba unga na kuwa mfanyabiashara mzuri tu lakini nimeacha kwani niligundua ni biashara mbaya sana na naomba Mungu anisamehe.
Ijumaa: Nani alikushawishi kuingia katika biashara hiyo mbaya?
Lungi: Ni rafiki yangu mmoja hivi ila siwezi kumtaja, najuta na sitarudia tena.
Ijumaa: Kwa kufanya biashara hiyo ulinufaikaje na unawashauri nini wale wanaotamani kufanya kazi hiyo wakiamini watapata mafanikio ya haraka?
Lungi: Kimsingi sijafaidika sana, ni kazi hatari ambayo simshauri mtu kuifanya. Si wanasikia yanayowakuta watu wanaogeuzwa punda?
Ijumaa: Ushawahi kutoa mimba?
Lungi: Sijawahi, mimi naona ni uuaji.
Ijumaa: Unatajwa kuwa mmoja wa mastaa wenye tabia ya kuwaunganisha wenzako kwa wanaume, hili nalo likoje?
Lungi: Ilikuwa zamani lakini sasa nimeacha, nimeona ni kazi isiyo na manufaa kwangu.