Wednesday, February 11, 2015

Mwalimu Apandishwa Kizimbani kwa Kupora Mume wa Mtu


MWALIMU wa Shule ya Msingi Manga katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Mary Majilanga amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Utemini, mjini Singida kujibu shitaka la kukamatwa ugoni .
 
Katika kesi hiyo ya madai namba 8 ya mwaka huu, mshitakiwa Mary anatakiwa kulipa Sh milioni 8 za ugoni kwa kuishi kama mume na mke na mwalimu mstaafu, Julius Magandi ambaye imeelezwa ni mume wa Severina Michael Kisunga waliojaliwa kuwa na watoto watano tangu ndoa yao mwaka 1985.
 
Licha ya kufunguliwa kwa kesi hiyo ya madai Januari 26 mwaka huu na kutolewa hati ya kuitwa shaurini mara mbili, mshitakiwa amekuwa hahudhurii mahakamani badala yake Magandi amekuwa akipeleka taarifa mahakamani kuwa mshitakiwa ni mgonjwa.
 
Hata hivyo juzi wakati kesi hiyo ikitajwa mbele ya Hakimu Fedinand Njau, baada ya Magandi kusimama tena mahakamani na kudai mshitakiwa yupo hospitalini anatibiwa, Hakimu Njau alimpa Magandi dakika tano kuhakikisha anamleta mshitakiwa mahakamani.
 
Baada ya nusu saa kupita hatimaye Magandi aliwasili mahakamani hapo akiwa ameongozana na mshitakiwa na alipopandishwa kizimbani mshitakiwa alidai kuwa alikuwa hospitali ya mkoa kutibiwa macho.
 
Akijibu shitaka la kukamatwa ugoni, mshitakiwa Mary alidai kuwa mwanaume Julius Magandi anayedaiwa kukamatwa naye ugoni ni mume wake halali na kwamba wamefunga naye ndoa ya kimila tangu 2013.
 
Naye Magandi alidai kuwa Mary ni mke wake wa pili aliyefunga ndoa ya kimila baada ya kuasi Ukristo na kuamua kuibadili ndoa yake ya kanisani ya mke mmoja kuwa ya wake wengi.
 
Kutokana na Hakimu mwenye jalada la kesi hiyo kuwa safarini Dodoma kikazi, Hakimu Njau aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.