Friday, March 27, 2015

WEZI WA MIFUGO WAUAWA KWA KUCHOMWA MOTO HUKO MARA


Watu watano wamekufa katika matukio matatu tofauti, wakiwemo watatu waliouawa na miili yao kuchomwa moto na wananchi wanaojiita wenye hasira, baada ya kutuhumiwa kuiba ng’ombe 40 katika Wilaya ya Bunda Mkoani Mara.
 
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philipo Kalangi, tukio la kwanza lilitokea Machi 24 mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha Kunanga wilayani Bunda.
 
Alisema watu hao watatu waliuawa kwa tuhuma ya kuiba ng’ombe 40, mali ya Julius Malima (56), mkazi wa kijiji cha Kenkombyo- Neruma kata ya Neruma wilayani Bunda, baada ya kuvunja zizi na kuanza kuswaga ng’ombe hao, majira ya saa 10:00 usiku.
 
Alitaja waliouawa kuwa ni Mayala Buluma (29) mkazi wa kijiji cha Jiniva-Kyabakari Wilaya ya Butiama na Mukina Buluma (25), mkazi wa kijiji cha Namhura wilayani hapa, ambao wote ni watoto wa mzazi mmoja.
 
Mwingine ni Chacha Masagati (22), mkazi wa kijiji cha Kyabakari Wilaya ya Butiama.