Shule mbalimbali za sekondari za bweni zinazomilikiwa na Serikali zimefungwa kutokana na kukosa chakula.
Uchunguzi umebaini takribani kwenye mikoa yote kuna shule zimefungwa na nyingine ziko hatarini kufungwa kwa kukosa chakula.
Mkoani Dodoma Shule ya Sekondari Mpwapwa iliyopo katika Wilaya ya Mpwapwa ilitakiwa kufunguliwa tangu Aprili 8, lakini imeshindikana kutokana na ukosefu wa chakula.
Mkuu wa shule hiyo, Nelson Mbilinyi, alisema walifunga shule kwa ajili ya likizo fupi, lakini hadi sasa hawajajua ni lini watafungua kutokana na tatizo hilo.
Mkoani Tabora, shule nne zimefungwa kutokana na wazabuni kusitisha huduma kutokana na kuidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 1.5 za chakula walichokisambaza kwa shule mbalimbali.
Sekondari zilizofungwa ni Kazima ambayo wanafunzi wote wamerudishwa makwao isipokuwa wale wa kidato cha sita ambao wamepewa maelekezo ya kuwa wavumilivu kwani watabaki wakijiandaa kwa ajili ya kufanya mitihani.
Shule nyingine iliyofungwa ni Sekondari ya Tabora Boys ambapo kwa mujibu wa mwalimu ambaye hakutaka kutaja jina lake, wanafunzi wote wamerudishwa majumbani kwao na kubakishwa wa kidato cha sita tu wanaojiandaa kwa mitihani yao ya mwisho.
Sekondari nyingine ambazo pia zimefungwa kutokana na kadhia hiyo mkoani humo ni pamoja na Milambo na Tabora Girls ambazo idadi ya wanafunzi waliorudishwa makwao haijafahamika.
Katika Mkoa wa Mtwara, taarifa zinasema shule za sekondari zilizopo wilayani Masasi tayari zimefungwa kutokana na hali hiyo.
Shule hizo zimetajwa kuwa ni Ndanda Boys, Masasi Girls, Chidya na Ndwika.
Katika Mkoa wa Mwanza, wazabuni wa vyakula mashuleni wametishia kugoma kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh milioni 800.
Shule ya Sekondari Mwanza, iliyopo katika Wilaya ya Nyamagana inadaiwa na mzabuni kiasi cha Sh milioni 116, ambazo ameshindwa kulipwa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.
Shule nyingine ambazo zinadaiwa na wazabuni ni Sekondari yaNsumba pamoja na Ngaza, ambapo taarifa za uhakika zinaeleza kuwa kwa ujumla wake zinadaiwa zaidi ya Sh milioni 300.
Mkoani Arusha nako hali si shwari baada ya shule za Ilboru, Longido, Engutoto, Makuyuni na Kisimiri kudaiwa kuwa katika hali mbaya kutokana wazabuni kudai mamilioni ya fedha.
Mkoani Mbeya, Shule ya Sekondari ya Iyunga, inatarajiwa kufungwa leo, kutokana na ukosefu wa chakula.
Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Edward Mwakimwa, alikiri kukabiliwa na uhaba wa chakula na kusema tayari uongozi wa shule kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa unaendelea na mchakato wa kuhakikisha chakula kinapatikana kwa wakati.