Monday, May 11, 2015

COUTINHO HATARINI KUTEMWA YANGA SC KUMPISHA MSHAMBULIAJI TISHIO AFRIKA

YANGA SC huenda itamuacha kiungo Mbrazil Andrey Coutinho ili kusajili mshambuliaji wa kigeni mwenye uwezo mkubwa wa kukidhi ushindani wa michuano ya Afrika.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Yanga SC zinasema kwamba benchi la Ufundi linaridhishwa na uwezo wa Coutinho, lakini linaamini wachezaji wa aina yake na nafasi yake wapo wengi nchini.
“Mawinga wazuri kama au kuliko ni yeye ni wengi hapa Tanzania, lakini kupata mshambuliaji wa kiwango cha juu hapa Tanzania ndiyo shida,”kimesema chanzo kutoka Yanga.
Coutinho aliyekuja nchini pamoja na Mbrazil mwingine, Geilson Santana Santos ‘Jaja’ aliyeondoka Desemba baada ya kufunga mabao matano katika mechi 11- alianza vizuri kabla ya baadaye majeruhi kumpunguza kasi.
Andrey Coutinho anaweza kutemwa Yanga SC ili ipatikane nafasi ya kusajili mshambuliaji mkali

Hadi sasa, Coutinho ambaye alikwishaanza kujizolea mashabiki kibao Yanga SC, amefunga mabao sita katika mechi 25 za mashindano yote.
Tayari Yanga SC imekwishafikia makubaliano na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma anayechezea klabu ya Platinum Stars ya huko aje Dar es Salaam.
Ngoma amekubaliana kila kitu na Yanga SC na sasa kilichobaki na klabu hizo mbili kumalizana. 
Wakati Coutinho aliyesajiliwa msimu huu chini ya kocha Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo yuko hatarini kutemwa, viungo wengine wawili wa kigeni, Mbuyu Twite kutoka DRC na Haruna Niyonzima wa Rwanda wote mikataba yao imekwisha.
Wachezaji hao wote ni muhimu kwenye kikosi cha mabingwa hao wa Bara na wamo kwenye mipango ya msimu ujao ya benchi la Ufundi chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm, anayesaidiwa na mzalendo Charles Boniface Mkwasa.
Mshambuliaji Kpah Sherman kutoka Liberia atapewa nafasi nyingine baada ya kuanza vibaya katika msimu wake wa kwanza, akifunga mabao sita katika mechi 22 za mashindano yote.
Kiungo wa kimataifa wa Seirra Leone, Lansana Kamara yupo Dar es Salaam kwa ajili ya majaribio Yanga SC.
Kijana huyo mdogo mwenye umri wa miaka 22, amekuja Tanzania akitokea Sweden ambako amechezea klabu za Umea FC aliyojiunga nayo Januari 1, mwaka huu akitokea Vimmerby IF iliyomsajili Machi 12, mwaka jana.
Awali ya hapo, Kamara alichezea pia Eskilstuna City FK tangu Jan 1, mwaka 2013 akitokea  Vimmerby IF, klabu yake ya kwanza nchini humo tangu aondokea kwao kwenda kutafuta maisha Ulaya.
Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaruhusu wachezaji watano tu wa kigeni na Yanga SC ilimaliza msimu ikiwa imetimiza idadi hiyo kutokana na Niyonzima, Twite, Coutinho, Sherman na Mrundi Amissi Tambwe- maana yake italazimika kukata mchezaji ili kuongeza mgeni mwingine.