Gumzo la mjini wiki hii ilikuwa ni shoo ya mchumba wa Nasibu Abdul ‘Diamond’ Zarinah Hassan ‘Zari’ iitwayo Zari All White Party iliyofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar na ile ya Instagram Party ambayo ilimhusu mrembo Wema Sepetu iliyofanyika jijini Mwanza ambapo nyuma ya pazia, warembo hao walitoana jasho kuhakikisha wanafunikana, Risasi Jumamosi lina stori kamili.
MVUTANO WAANZA
Kwa mujibu wa chanzo, mvutano wa Wema aliyewahi kuwa mchumba wa Diamond na Zari ambaye anammiliki Diamond kwa sasa, uliibuka Alhamisi iliyopita wakati kila mmoja akijiandaa kwenda kwenye shoo inayomhusu.
“Wema na Zari leo ni full kutoana jasho, kila mmoja anataka kuwavuta mashabiki wengi upande wake.
ZARI APEWA SAPOTI
“Zari amepata sapoti kubwa kutoka kwa mpenzi wake wa sasa Diamond kwani walikuwa wanafanya shoo pamoja hivyo alikuwa na kibarua cha kuwakusanya mashabiki wote wa Diamond waende kwenye shoo yake ili Wema asipate watu,” kilisema chanzo hicho.
UPANDE WA WEMA
Chanzo hicho kilizidi kumwaga ubuyu kuwa, kwa upande wa Wema, yeye alikuwa na kibarua kizito cha kuwakusanya marafiki zake hususan mastaa wa Bongo Movies wasiende kwa Zari na badala yake waende Mwanza kwenye Instagram Party.
“Ni mnyukano wa aina yake, Wema alikuwa na kibarua kizito kuwashawishi Bongo Movies waikache shoo ya Zari waende Mwanza kwenye Instagram, bahati nzuri alifanikiwa kwani wasanii wengi walimuunga mkono,” kilisema chanzo hicho.
MATUSI
Hadi jana jioni, kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Timu ya Zari (Team Zari) na ile ya Wema (Team Wema) zilikuwa zikirushiana matusi huku kila mmoja akionesha hisia zake.“Hakuna kwenda kwa Zari, twendeni kwa Wema Mwanza, watakaokwenda kwa Zari ni wapuuzi kabisa,” ilisomeka moja ya komenti ya mdau wa timu Wema huku timu Zari ikijibu:“Wajinga wakubwa watakaokwenda kwa Wema, mpango mzima ni kwa Zari na Diamond pale Mlimani City.”
STEVE AFUNGUKA
Ili kuzidi kupata data zaidi, wanahabari wetu walimtafuta mdau mkubwa wa kuwashawishi watu, mwigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ ambaye aliweka bayana kuwa wao kama Bongo Movies, wanamuunga mkono Wema.
“Niweke wazi tu kwamba sisi tutakwenda kwa Wema, hii shoo ya Zari na Diamond itatupitia kushoto kwa kweli,” alisema Steve.
KAJALA KWA ZARI
Kwa upande wake Kajala Masanja alikuwa tofauti na waigizaji wenzake ambapo alipokea kwa mikono miwili mwaliko wa Zari na kuanza kuihamasisha Team Kajala kwenda kwenye shoo hiyo.
WEMA AFUNGUKA
Jitihada za kumpata Zari aweze kufungukia mvutano huo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kuita bila majibu lakini bahati nzuri Wema alipatikana na kufunguka:“Mimi kama mimi nakwenda katika shoo inayonihusu ya Instagram, hiyo ya Zari siijui. Sijashawishi mtu ila watu wameamua kuniunga mkono, siwezi kuwazuia na hao wanaofikia hatua ya kutukana pia siwezi kuwazuia,” alisema Wema.
MWISHO UKOJE?
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, shoo ya Zari ilitarajiwa kurindima na mashabiki wake huku Wema akiwa na mashabiki wake waliomuunga mkono hivyo kusababisha mtikisiko wa aina yake mjini.