WAKATI ugawaji wa majimbo 211 ukikamilika kwa vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa), imebainika kwamba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibuka na asilimia 50 katika majimbo hayo.
Chama kilichofuata ni Chama Cha Wananchi (CUF) ambacho kinadaiwa kupata asilimia 35-40, NCCR-Mageuzi asilimia 10 huku NRD kinachoongozwa na Emmanuel Makaidi kuachiwa asilimia 1-2.
Taarifa ambazo MPEKUZI imedozwa zinadai kuwa mgawanyo huo umefanywa kwa kuzingatia vigezo vya nguvu za kila chama katika eneo husika.
“Ndiyo maana umeona huu mchakato umechukua muda mrefu kwasababu ilikuwa inafanyika tathimini kuona nani ana nguvu wapi na nani ana nguvu eneo gani mwisho wa siku umeona kwa haya 211 wamekubalina,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe.
Akizungumzia majimbo 12 yaliyoleta utata anasema “Majimbo haya ni sita ya hapa Dar es Salaam ambayo kuna Segerea, Temeke, Ukonga, Ilala na Kinondoni.
“Kwa mikoani kuna jimbo la Serengeti, hili linaleta utata kwasababu kuna mvutano kati ya watu wa Chadema na katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi Mosena Nyambabe ambaye analitaka lile jimbo.
“Lakini taarifa zilizopo ni kwamba Nyambabe aliangukia pua katika uchaguzi wa serikali za mtaa na Chadema waliibuka kidedea, sasa ameambiwa kuachia jimbo lakini yeye hataki, ndiyo na lenyewe limewekwa kiporo.
Taarifa hizo zinaendelea kudai kuwa jimbo jingine lililotea mgogoro ni Vunjo linaloshikiliwa na TLP ambapo tayari Mwenyekiti wa NCCR-James Mbatia tayari ameonyesha nia ya kugombea.
“Huku nako kuna mgogoro mwingine kwasababu tayari Mbatia ameshatangaza nia na amefanya kazi kubwa katika jimbo hilo, lakini kuna kada mkubwa wa Chadema aliyewahi kugombea jimbo hilo naye ameweka msimamo kwamba ni lazima agombee."
Majimbo mengine yanayotajwa kuweka umoja huo njia panda ni pamoja na Mtwara mjini na Mafia ambapo taarifa kutoka kwa kiongozi mmoja wa Ukawa zinasema kuwa wamepeana siku kumi kuanzia leo (jana) kwa kila kiongozi kuhakikisha amekamilisha mchakato wa kukamilisha utaratibu kwa majimbo yaliyobaki.
Katika makubaliano Jimbo la Vunjo liliachwa mikononi mwa NCCR-Mageuzi ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia amejinadi kulichukua kutoka mikononi mwa mbunge wa sasa Agustino Mrema.
Akizungumzia Makaidi kupewa asilimia moja mpaka mbili alisema kuwa inatokana na mzee huyo kuonyesha msimamo ndani ya umoja huo.
“Makaidi hakuonyesha tamaa kama viongozi wengine wa upinzani baada ya kususia kwenye Bunge la Katiba, hakuonyesha tamaa ya kutaka posho za Bunge la Katiba, aliweka msimamo hadi leo hii, kwahiyo ndani ya Ukawa Mzee Makaidi ameonekana shujaa."
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa Chadema ndiyo chama chenye nguvu ndani ya Ukawa ambapo taarifa za ndani zilidai kuwa katika mchakato wa kugawana majimbo kulikuwa na mvutano mkali huku chama hicho kikitaka kuachiwa majimbo mengi hali iliyobua mgogoro kutoka katika vyama vingine.
Lakini duru za kisiasa zinaendelea kuonyesha kuwa mgawanyo huo pia unaweza usieleweke kwa wanachama wa kawaida wa Chadema wakiwemo wabunge wao ambao wanashikilia majimbo mbalimbali.
MPEKUZI imepata mawasiliano ya kundi moja la wabunge wa Chadema wanalolitumia katika mtandao wa kijamiii likionyesha kushangazwa na baadhi ya vyama kutaka majimbo wanayoyashikilia.
Wabunge walioshiriki mjadala huo walionyeshwa kushangazwa na kitendo cha CUF kuomba kuachiwa baadhi ya majimbo wanayoyashikilia huku wengine wakionyesha shaka kwamba inawezekana ni njia ya chama hicho kutaka kuvunja umoja huo.
Katika kuonyesha kukasirishwa mmoja wa wabunge alikwenda mbali zaidi na kutoa angalizo kwa viongozi wao wa juu kuacha kuwaendekeza CUF huku mwingine akipendekeza chama hicho kuwaachia Chadema majimbo ya Zanzibar.
Mbunge huyo aliyataja majimbo ya Zanzibar ambayo wangependa waachie kuwa ni pamoja na Pemba na mji mkongwe.
Mwingine aliyechangia katika majadala huo alisema CUF wana undugu na CCM isije ikawa wametumwa kuubomoa Ukawa, huku mwingine akichangia kwa kusema kama ni mkakati wa kuingia Ikulu kwa upinzani ni sawa lakini kama siyo hivyo kuna sababu za kubishana kulinda majimbo yao.
Majimbo yaliyotajwa kumezewa mate na wabunge hao ni Musoma Mjini,Nyamagana na majimbo mengine mengi huku mmoja wa wabunge waliokuwa wakishiriki mjadala katika kundi hilo alisema kwa muktadha huo Ukawa ni shiidaa huku mwingine akisema ni matusi kwa CUF kutaka majimbo yao.
MPEKUZI ilipata wakati mgumu wa kuwapata viongozi hao wa Ukawa kwani hata wale waliofikiwa wamekataa kuzungumzia jambo hilo huku taarifa zikidai kuwa wamepeana onyo kali katika vikao vyao kuhakikisha hakuna anayetoa taarifa za vikao nje.
Katika mkutano wa Juzi, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema Ukawa iko imara sasa kuliko kipindi cha nyuma na alikanusha chama chake kuandika barua ya kujiondoa katika umoja huo.
Ukawa ni muungano wa vyama vinne vya upinzani ambapo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NRD.
Muunganiko huo ulifanyika katika Bunge la Katiba ambapo lengo lake kugomea Katiba Pendekezwa wakiamini wanaburuzwa na chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo baadaye waliamua kuendeleza umoja huo katika mambo mengine ya Urais.