Wednesday, May 27, 2015

Mke amkodia Mchepuke wa Mumewe KIBAO KATA kumsuta akiwa Kazini...Matukio katika Picha

 
MWANAMKE mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja, mwishoni mwa wiki iliyopita alijikuta katika wakati mgumu baada ya kundi la wanawake kumvamia kazini kwake na kuanza kumsimanga kwa kitendo chake cha kuchepuka na mume wa mtu huku akipigiwa ngoma maarufu kama kibao kata. 
Wakimsimanga kwa staili ya kusasambua.
Tukio hilo lilitokea Mei 23 mwaka huu maeneo ya Kimara Mwisho, ambapo awali mke wa mume aliyechepuka, aliyejitambulisha kwa jina moja la Upendo, alidai mara kwa mara amekuwa akipokea taarifa kuwa mwanamke huyo anatembea na mumewe jambo lililomfanya amtafute, lakini alikataa katakata, akidai wao ni marafiki wa kawaida.
Akizungumza na waandishi wetu, mke huyo wa mtu alisema baada ya kuzungumza na mumewe mambo hayo yaliisha, lakini siku chache zilizopita aliiona simu ngeni ndani ya gari la mumewe, alipoipiga akagundua kuwa ni ya mwanamke huyo, jambo lililoibua upya mgogoro baina yao.
Ngoma ya kibao kata ikilindima wakati wa zoezi hilo.
“Nilimalizana na mume wangu lakini safari hii nikampigia simu yule mwanamke na kumpa tahadhari, lakini majibu aliyonipa nilipata hasira sana, eti alisema kama namchunga sana mume wangu basi nimjengee zizi nimfungie. Nikaona hizo ni dharau, nikaamua lazima nimsute,” alisema Upendo.
Kama  hiyo haitoshi mke huyo wa mtu alisema kuwa siku moja alipata taarifa kuwa mumewe amepigwa chupa na mchepuko huo, kisa kikiwa ni wivu wa kimapenzi ambapo katika sekeseke hilo gari yake ilivunjwa kioo jambo lililomzidisha hasira kiasi cha kumtafutia kibao kata.
Waandishi wetu waliokuwa katika kusaka matukio walilinasa tukio hilo ambapo walishuhudia umati wa kina mama wa mjini walioshushwa eneo hilo kutoka kwenye gari aina ya kirikuu, wakimvaa mwanamke huyo aliyekuwa saluni kwake bila habari kama ngoma hiyo imemfuata ili asutwe na mwenye mali.
Mke anayedai kuibiwa mumewe.
Katika hali ya kushangaza, ghafla aliwachoropoka na kutoka mbio kukimbilia chooni katika nyumba ya jirani na kujifungia ndani  huku juhudi za kumtoa zikishindikana.
Kama hiyo haitoshi ngoma ya kibao kata iliendelea kupigwa huku wakina mama wakimwaga radhi waziwazi, wakimchamba vilivyo huku mtaa ukiwa umefungwa kwa muda, kuhakikisha tabia ya mwanamke huyo inajulikana mtaa mzima hali iliyofanya umati wa watu kujaa wakitaka kushuhudia nini kinachotokea eneo hilo.