Thursday, May 21, 2015

STEVE NYERERE ANADAIWA KULAMBA FEDHA ZA KABURI!

Waandishi wetu
TAKRIBAN mwaka mmoja tangu mwigizaji Adam Kuambiana aiage dunia, kaburi lake limeibua skendo ya wasanii kudaiwa ‘kuchikichia’ fedha za kulijengea, Amani lina full stori.
Mwigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ akiwa kwenye kaburi la marehemu Kuambiana.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini, kaburi la nguli huyo wa sinema lilipokuwa linatimiza mwaka mmoja, ilidaiwa lilitoka fungu la shilingi milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ili zijengee kaburi hilo lakini zikazuiwa kwanza kwenye mifuko ya mwigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’.
“Wiki moja kabla ya shughuli ya misa ya kutimiza mwaka mmoja kifo cha marehemu, Nyerere (Steve) alipewa alipewa shilingi milioni moja, akakaa kimya hadi kaburi likajengwa na mke wa marehemu Julieth Lite (Diwani wa Kunduchi) kwa kutumia fedha zake,” kilisema chanzo hicho.
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.
UBUYU WAZIDI KUMWAGWA
Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, siku moja kabla kumbukumbu iliyofanyika Jumapili iliyopita (Jumamosi), mjane wa marehemu alipokea shilingi laki saba kutoka kwa mtu aliyejisajili kwa jina la Albert Msando akimwambia ni mchango wa Makonda wa kujengea Kaburi.Baadaye iliingia shilingi laki tatu kwenye namba nyingine ya simu ambayo ilielezwa kuwa ni mchango wa kujenga kaburi uliotoka kwa mwigizaji Jacob Steven ‘JB’.
STEVE NYERERE AJINADI
Wakati maandalizi ya misa yakiendelea, Jumamosi jioni, Steve Nyerere na baadhi ya wasanii walitupia picha kwenye mtandao wa kijamii huku wakisindikiza na ujumbe uliojinasibu kuwa wanamshukuru Mungu kuashiria wamefanikisha kujengea kaburi hilo kitu ambacho kilikanushwa baadaye na mwigizaji Kulwa Kikumba ‘Dude.’
“Jamani hakuna msanii aliyehusika kujengea kaburi zaidi ya mke wa marehemu, Julieth Lite,” aliandika mitandaoni Dude ambaye ni mdogo wa Julieth.
Mwigizaji Kulwa Kikumba ‘Dude.’
MJANE AFUNGUKA
Amani lilimvutia waya mjane wa marehemu Kuambiana, Julieth ambaye naye alisisitiza kuwa kaburi hilo alilijenga kwa fedha zake mwenyewe.“Nilijenga mwenyewe lakini wakati tunakaribia kufanya misa (Jumamosi) nakumbuka ilikuwa kama saa tano na nusu usiku,  ghafla nilipokea shilingi laki saba kutoka kwa Msando nikaambiwa ni za Makonda na baadaye nikapokea laki tatu nikiaambiwa ni za JB,” alisema Julieth.
NYERERE ANASEMAJE?
Amani lilipomtafuta Steve Nyerere na kuulizwa kama ni kweli alipewa shilingi milioni moja na Makonda kisha akakaa kimya na kama zile laki saba zilizokabidhiwa na Msando zinahusiana na zile alizopewa na Makonda, alijibu:
“Ninavyojua mimi hizo fedha hajatoa Makonda, tumetoa sisi wasanii kama huamini ongea na JB huyu hapa (akampa simu).
“Tulitoa sisi wasanii, kama ulikuwepo siku ile pale makaburini ungeona alichoongea mke wa Kuambiana. Ni sisi kaka ndiyo tumetoa. Wewe mpigie mke wa marehemu halafu muulize alichosema siku ile makaburini halafu nipigie tena,” alimalizia JB na kukata simu.
Alipopigiwa Makonda ili aweze kudadavua kiundani juu ya fedha alizotoa na nani aliyempa alijibu:
“Nipo katika kikao unaweza kunitumia meseji?”
Licha ya kutumiwa meseji, hadi tunakwenda mitamboni, hakuwa ametoa jibu lolote.