Saturday, June 13, 2015

CHEZEA JESHI WEWE:KUMBUKUMBU YA JESHINI YAMLIZA JB

Jacob Steven Mbura ‘JB’.
JACOB Steven Mbura ‘JB’ anaendelea kusimulia historia ya maisha yake tangu utotoni hadi sasa. Ni simulizi ndefu na tamu isiyochosha kwa vimbwanga na kila aina ya mikasa ya kusisimua na kustaajabisha. Uhondo huu una takriban wiki tatu sasa, na amefikia kwenye kipengele cha maisha yake jeshini ambapo alieleza sulubu ya mikikimikiki ya jeshini huku akikiri kwamba jeshi lilimkomaza.Je, nini kinaendelea? Jikongoje nayo sasa...
“Kama nilivyoanza kueleza hapo awali kuwa, maisha ya jeshini yalinibadili kwa kiwango kikubwa mno,” aliendelea JB.
“Mikikimikiki ikaendelea kuwa mingi, karibu kila mmoja wetu tulioingia pamoja alikuwa ameshaanza kuyazoea maisha hayo,” anasimulia.
“Nasimulia historia hii ya maisha yangu, hususan maisha ya jeshini hakika nakumbuka mbali sana na wakati mwingine narudisha hisia nyuma na kuyaona maisha jinsi yanavyobadilika,” alisema JB kwa sauti ya chini huku akionesha sura ya masikitiko kidogo.
“Mbona umeonekana kubadilika ghafla kwa kuonesha huzuni namna hii kaka?” nilimtupia swali hilo wakati nikimsogelea karibu zaidi na kumtazama machoni bila kuyapepesa macho yangu.
“Haaa..., unajua nakumbuka mbali sana, natamani kukutana mahali fulani na watu wote ambao tulikuwa pamoja jeshini, natamani tukutane tena pamoja mahali fulani na tuwe na maisha yale,” alisema mfululizo JB kwa hisia kali sana huku akiuma kidole kidogo cha mkono wa kulia na kusonya mara nyingi kwa wakati mmoja.
Hapohapo, napata munkari zaidi wa kujua mengi zaidi kuhusu JB.
“Kwa ni nini uwe na shauku ya kukutana na watu uliokuwa nao jeshini tu na si sehemu nyingine kama shuleni,” nilimuuliza wakati nikiitazama kalamu yangu kwa umakini kwa kuikagua kama iko ‘fiti’ kudondosha wino unaotokana na maneno matamu na ya kusisimua kutoka mdomni mwa mfalme huyu wa filamu kwa sasa, JB katika ubora wake.
“Ni kweli nimepitia maeneo mengi na kukutana na watu wengi mno tofauti, lakini kampani ya watu niliokutana nao jeshini, hakika ilikuwa ni zaidi ya furaha, ucheshi, mshikamano, ushirikiano, kusaidiana na kila aina ya furaha ya maisha ilipatikana jeshini kwa jamaa niliokuwa....!
JB anashindwa kumalizia sentensi hiyo, ghafla namuona akisitisha kabisa mazungumzo, natazama pembeni kidogo, natulia na kisha kumtazama tena.
“Kaka, kaka, kaka, vipi tena,” niliita na kumuuliza nikitarajia huenda angeendelea na simulizi.
Haikuwa hivyo. Nikamuona akiinamisha kichwa katikati ya mapaja yake, na haraka sana akatoa kitambaa chake cha gharama na kujifuta usoni!
Ni hapo ndipo niligundua kuwa JB alikuwa akidondosha machozi. Ndiyo, tena machozi ya hisia kali, jambo lililonifanya nibaki nimeduwaa! Alikuwa akilia! Akiyalilia maisha ya jeshini!
“JB mbona unalia sasa?” nilimuuliza.
“Acha tu mdogo wangu, kama kuna mtu niliyekuwa naye jeshini huko Kabuku Tanga kwa wakati huo na atabahatika kusoma gazetini simulizi yangu kwa maisha ya jeshini, atakuwa shahidi wa nilichokisema, yalikuwa ni maisha ambayo tangu hapo sijawahi kukutana nayo maishani tena, na sijui kama nitakutana nayo tena,” anabainisha JB na kuendelea kujifuta machoni huku!
“Kwa sasa wengine wapo, tena ni viongozi wa ngazi za juu mno serikalini, lakini kuna waliokwisha tangulia mbele ya haki, maisha yamebadilika sana na nikuambie kitu mdogo wangu?” anasema JB na kisha kunitupia swali hilo.
Wakati najiandaa kumjibu, namuona aki...
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose wiki ijayo!