Friday, June 26, 2015

Huu ndio ugumu wa LOWASA Kupenya kwenye URAIS

30Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa.

VUGUVUGU la watangaza nia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchuana kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa rais, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu linazidi kuwa kubwa kila kukicha.
Idadi ya makada wa chama hicho wanaowania nafasi hiyo, inazidi kuongezeka ambapo mpaka sasa, zaidi ya makada 40 wamejitokeza kwenye makao makuu ya chama hicho, Dodoma na kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
Licha ya utitiri huo wa wagombea, mtu anayetakiwa ni mmoja tu na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo wanavyozidi kuibuka watu wanaobadili kabisa upepo wa kisiasa ndani ya chama hicho, wengine wakipewa nafasi kubwa huku wengine wakionekana kuwa ‘mamluki’ katika safari hiyo ya kuelekea Ikulu .
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa, ni kada ambaye mpaka sasa, nguvu zake za ushawishi miongoni mwa wananchi na wanachama wa chama hicho zimejipambanua pengine kuliko mgombea mwingine yeyote, huku akipewa nafasi kubwa ya kurithi kiti kitakachoachwa wazi na swahiba wake wa siku nyingi, Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Hata hivyo, licha ya dalili zote za awali kuonesha kwamba Lowassa ana nafasi kubwa ya kuteuliwa na chama hicho, hasa kutokana na jinsi anavyokubalika miongoni mwa wananchi, akifunga mitaa kila anapokwenda kuomba udhamini mikoani, duru za kisiasa ndani ya chama hicho, zinaonesha kwamba uwezekano wa mbunge huyo wa Monduli kupenya ni mgumu kutokana na sababu kadha wa kadha.
Kwa mujibu wa Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alizungumza kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mfumo usio rasmi utakaotumiwa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kuwachuja wagombea hao ili kumpata mmoja atakayekiwakilisha chama, unaonesha ‘kutokuwa rafiki’ kwa Lowassa.
MFUMO UTAKAOTUMIKA
“Unajua chama tawala kinatumia mfumo wa ‘X, 5, 3, 1’, yaani maana yake ni kwamba watajitokeza watangaza nia wengi ambao idadi yao haina kikomo (X) ambao sekretarieti kuu ya chama itayapitia majina yote kisha kuyapeleka kwenye Kamati Kuu (CC) ambayo itayachuja majina hayo kwa kuzingatia vigezo 13 vilivyowekwa na chama ili kupata majina ya wagombea watano watakaopelekwa kwenye Halmashauri Kuu.
“Majina hayo matano yatachujwa na Halmashauri Kuu ili kupata majina matatu ambayo yatapelekwa kwenye mkutano mkuu wa chama utakaopitisha jina moja kwa hiyo kanuni ya ‘X, 5, 3, 1’ itakuwa imetimia,” alisema profesa huyo.
UGUMU UNAANZIA HAPA
Profesa huyo aliliambia Uwazi Mizengwe kwamba ugumu kwa Lowassa kupenya kwenye mchujo huo, unatokana na sababu zifuatazo:
“Unajua hiki ninachowaambia siyo rasmi lakini ndiyo utaratibu utakaotumika na kama hamuamini mtajionea wenyewe. Katika majina matano yatakayopitishwa na Kamati Kuu, uwezekano mkubwa ni kwamba chama kitazingatia mambo kadhaa.
“La kwanza ni suala la             Muungano, ili kuulinda muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, lazima nafasi mbili kati ya tano za watakaopitishwa, zitatoka kwa wagombea wa Zanzibar ambapo mpaka sasa, uwezekano mkubwa unaonesha Makamu wa Rais, Mohamed Ghalib Bilal na Jaji Mstaafu, Augustino Ramadhan ndiyo wanaopewa nafasi.
“Pili chama kitazingatia suala la jinsia ambapo lazima katika nafasi hizo tano, moja itaenda kwa mwanamke. Habari za chini kwa chini zinaonesha Dk. Asha Rose Migiro ndiye mwenye nafasi kubwa ya kupita kwa kigezo cha jinsia, kwa hiyo katika zile nafasi tano, zinakuwa zimesalia nafasi mbili.
“Waziri mkuu ndiye mtendaji mkuu wa serikali, kwa lugha nyingine lazima awe ni mtu anayekubalika ndani ya chama kabla ya kupewa wadhifa huo mkubwa wa kumsaidia rais. Mizengo Pinda amekuwa waziri mkuu wa kipindi kirefu katika utawala wa Rais Kikwete tangu Lowassa alipojiuzulu.
“Kwa kuwa naye amechukua fomu, haitakuwa rahisi kwa wajumbe wa kamati Kuu ‘kumchinjia baharini’. Haipo rasmi lakini uwezekano mkubwa ni kwamba anaweza kubebwa na wadhifa wake ingawa suala la upendeleo ndani ya chama huwa halipewi kipaumbele.
“Kama ikitokea hivyo, maana yake, tayari kutakuwa na majina manne; Bilal, Jaji Augustino, Dk. Migiro na Pinda. Katika ile hesabu ya majina matano yanayotakiwa, inabakia nafasi ya mtu mmoja tu ambayo ndiyo hiyo itakayogombaniwa na akina Lowassa, Membe, Dk.Magufuli, Profesa Mwandosya, Wasira, Makamba na makada wengine wote waliosalia. Unafikiri itakuwa rahisi kwa Lowassa kupenya?” alisema profesa huyo.
UPEPO WA KISIASA ULIVYO
Licha ya ufafanuzi huo jadidi kutoka kwa mtaalamu huyo wa siasa, Uwazi Mizengwe lilienda mbele zaidi na kupima upepo wa kisiasa ulivyo miongoni mwa watangaza nia. Katika uchunguzi huo uliofanywa na gazeti hili, imebainika kwamba mpaka sasa hakuna mtangaza nia ambaye amekuwa gumzo kama ilivyo kwa Lowassa.
“Jamaa anakubalika sana, tuacheni utani. Yaani tangu siku ya kwanza alipotangaza nia pale Arusha, sote tuliona jinsi alivyokusanya umati mkubwa wa watu ambao haujawahi kutokea na hakuna mtangaza nia mwingine aliyevunja rekodi hiyo.
“Yote tisa, kumi ni ziara za mikoani kusaka wadhamini zinazofanywa na Lowassa. Yaani kila mkoa anaokanyaga, anapokelewa na maelfu ya wananchi na wanachama wa chama hicho. Maeneo yote aliyopita ameacha gumzo. Hiyo ni ishara kwamba Lowassa anakubalika sana,” alisema Profesa huyo, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Kama CCM wataamua kufumba macho na kutozingatia kigezo cha kukubalika, basi wanaweza kulikata jina la Lowassa lakini kama wataangalia mgombea anayeuzika kama Rais Kikwete alivyosema kwenye maadhimisho ya miaka 37 ya CCM kule Songea, ipo wazi kwamba Lowassa atapenya kwenye hatua zote za mchujo,” Ismail Mabula, mtaalamu wa siasa kutoka taasisi moja isiyo ya kiserikali iitwayo Free Political Forum, yenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam aliliambia Uwazi Mizengwe.
CCM WANASEMAJE?
Uwazi Mizengwe halikuishia hapo, liliwatafuta viongozi wa CCM na kutaka kujua wanazungumziaje mchakato huo. Kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho (jina limehifadhiwa) alipoulizwa kuhusu mchakato wa mchujo utakavyokuwa, alisema sifa na vigezo anavyotakiwa kuwa navyo mgombea vipo wazi na kwamba chama hicho kitasimamia kwa umakini utaratibu na kanuni.
Alisema CCM haitachuja wagombea nje ya kanuni na kwamba mgombea asiyekuwa na vigezo hatabakizwa kwa sababu ya cheo chake, hasa viongozi wa serikali kwani ni wadogo kuliko viongozi wa chama.
“Suala la kuteuliwa kutoka Kamati Kuu kwenda Halmashauri Kuu haliangalii vyeo, ukisema Waziri Mkuu na Makamu wa Rais wataingia kwa vyeo vyao utakosea kwa sababu kichama hao ni watu wadogo, kama utakumbuka katika uchaguzi wa mwaka 2005, John Malecela alikuwa Makamu Mwenyekiti wa chama lakini jina lake lilikatwa mapema.
“Vigezo 13 wanavyotakiwa kuwa navyo wagombea vipo wazi, tunasubiri muda tu ili tuanze kazi ya kuwachuja wagombea kumpata mmoja anayestahili kupeperusha bendera ya chama,” alisema ofisa huyo mwandamizi wa chama.
Kwa mujibu wa ratiba, mchakato wa kuchukua fomu utafikia mwisho Julai 2, mwaka huu kisha vitafuata vikao mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea kwa kuanza na kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili, Julai 8.
Kikao hicho kitafuatiwa na kikao cha Kamati Kuu (CC), Julai 9 kisha Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 12 na 13, mwaka huu ambapo hapo ndipo jina la mgombea mmoja atakayechaguliwa litakapotangazwa