Monday, June 8, 2015

MAKOSA 10 MKATABA WA SIMBA, SINGANO

Ramadhani Singano ‘Messi’ akisaini mkataba wake na Simba.
Na Mwandishi Wetu
SAKATA kubwa linaloutikisa mpira wa Tanzania sasa ni ule mkataba kati ya kiungo Ramadhani Singano ‘Messi’ na klabu yake ya Simba.Messi anasema mkataba wake unaisha 2015, lakini Simba inasisitiza mkataba wao na Messi unaisha mwaka 2016, jambo ambalo linazua tafrani kubwa.
Mkataba wa Simba na Ramadhani Singano ‘Messi’ unaoishia 2016.
Championi Jumatatu lina kopi ya mikataba yote miwili, ule wa Simba unaomalizika Julai, 2016 na ule alionao Messi unaofikia tamati Julai, 2015. Mikataba yote inaanza Mei Mosi, 2013.
Katika mchanganuo wa mikataba hiyo, inaonyesha kuna makosa kadhaa na saba kubwa ndiyo yanayoweza kumfanya mtu yeyote aingiwe na hofu.Hata kabla ya TFF kukutana na pande hizo mbili kesho Jumanne, Championi Jumatatu linaainisha makosa katika mikataba hiyo miwili.
Mkataba wa Simba na Ramadhani Singano ‘Messi’ unaoishia 2015.
Moja:
Fonts; yaani muonekano au aina ya herufi zinavyokaa. Ukiangalia mikataba yote miwili zinapishana. Maana yake ule wa Messi na ule wa Simba ni mikataba miwili tofauti kabisa. Kama Messi ana kopi, hiyo ni ya mkataba upi? Nani kachakachua? TFF watatoa jibu kesho.
Mbili:
Saini za Messi, Joseph Itang’are (Makamu Mwenyekiti wa Simba), Evodius Mtawala (Katibu Mkuu Simba), zimesainiwa tofauti chini ya mkataba. Kwingine saini ya kulia ni Mtawala, kwingine saini ya upande huo ni Mzee Kinesi.
Tatu:
Namba tano na sita zimekuwa tatizo katika mikataba yote miwili. Katika ule wa Simba unaoisha 2016, kuna sehemu inaonekana ilikuwa tano, imelazimishwa kuwa sita. Ule wa Messi unaoisha 2015, kuna sehemu sita, inaonekana wazi imelazimishwa kuwa tano!
Nne:
Sahihi ya mwanasheria Mutakyamirwa Phillemon iliyo katika mikataba yote miwili inaonekana kuwa na tofauti kubwa. Je, ipi hasa ni sahihi?
Tano:
Sahihi za Mzee Kinesi katika mikataba yote miwili inaonyesha tofauti kubwa pia. Mwenyewe anaweza kusema yake ni ipi?
Sita:
Mihuri ya Klabu ya Simba iliyogongwa katika mkataba wa Messi na ule wa Simba, iko katika sehemu tofauti kabisa, ukilinganisha mikataba yote miwili.
Saba:
Muhuri wa mwanasheria Mutakyamirwa Phillemon pia umegongwa tofauti. Kwenye mkataba wa 2016 umelala, ule wa 2015 umenyooka. Sasa ‘photocopy’ ya Messi inafanana na upi, je, wake ndiyo sawa au orijino ndiyo umechakachuliwa?
Nane:
Sehemu ya mwisho ya mkataba, moja mwanasheria kasaini kushuhudia mkataba huo Mei Mosi, 2013 na upande mwingine Juni Mosi, 2013. Mwanasheria alisaini mkataba mara mbili, au tarehe zilichakachuliwa. Kwa nini sasa?
Tisa:
Ukurasa wa mwisho wa mkataba ambao unakuwa na saini za Messi, Mtawala na Mzee Kinesi ndiyo unaonekana kuwa na matatizo mengi zaidi kwa kutofautiana kabisa kwa ule unaoisha 2015 na ule wa 2016.
Kumi:
Saini za Mzee Kinesi kwenye 2016 na ukurasa wa mbele wa 2015 zinafanana kwa maana ya kuwa na apostrophe (kimkato cha juu) pale kwenye jina Itang’are. Kimkato hicho cha juu, kinakosekana kwenye saini ya ukurasa wa mwisho katika mkataba unaoisha 2015!