Tuesday, June 9, 2015

MESSI NA SIMBA SC ‘NGOMA DROO’ TFF, WARUDISHWA MSIMBAZI KUJADILI MKATABA MPYA WA 2015/2016, HUU WA SASA…

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Simba SC kuketi na mchezaji wake, Ramadhani Yahya (pichani kulia) Singano ‘Messi’ kujadili namna ya kuingia Mkataba mpya, baada ya pande zote kuafiki Mkataba wa sasa una hitilafu. 
Katika kikao cha leo, makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam, Simba SC iliwakilishwa na Mjumbe wa Kamati yake ya Utendaji, Collins Frisch wakati Messi aliandamana na Mussa Kisoky wa Chama cha Wanasoka Tanzania  (SPUTANZA).  
“Katika kikao cha leo pande zote zimeeleza kutambua utata ulio ndani ya mikataba iliyokuwepo ambayo kimsingi iliingiwa kabla ya uongozi wa sasa wa Simba SC,”amesema Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa.
Katibu huyo wa zamani wa Yanga SC, ameongeza kwamba kwa pamoja pande hizo mbili zimekubaliana kuanza mazungumzo ya makubaliano mapya kwa ajili ya Mkataba utakaoanza msimu mpya wa 2015/2016.
Aidha, Mwesigwa amesema TFF inazitaka klabu nchini kushirikiana na SPUTANZA na Bodi ya Ligi katika kuweka mifumo mizuri ya uingiaji mikataba na wachezaji, makocha na waajiri wengine.  
“TFF inao mkataba mama ambao klabu zote na wachezaji wanatakiwa waufuate wakati wanaandaa mikataba yao.  Aidha TFF inawataka  wachezaji kuelewa mikataba kabla ya kutia sahihi,”amesema Mwesigwa.
Katibu huyo ameongeza kwamba, TFF itazidi kuboresha mfumo wa usajili wa wachezaji na mikataba ili kuweka mazingira sawia kati ya pande zote mbili, wachezaji na klabu.
Barua ya hukumu ya kesi ya Messi na Simba SC leo

Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka minne iliyopita, hivi karibuni ameibua shutuma dhidi ya klabu yake hiyo kwamba imeghushi Mkataba wake.
Messi anadai Mkataba wake halali ulikuwa unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika mwakani.
Na Messi si mchezaji wa kwanza kuishutumu Simba SC kughushi Mkataba wake, kwani wachezaji wengine za zamani wa klabu hiyo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Kevin Yondan wamewahi kutoa malalamiko kama hayo wakati wanahamia kwa mahasimu, Yanga SC.