Tuesday, June 9, 2015

SIMBA SC ‘YAJITOA’ KOMBE LA KAGAME KISA TFF NA MKWARA WA YANGA

SIMBA SC haitashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kwa sababu mbili kubwa- hawajapewa taarifa yoyote hadi sasa na pili muda uliobaki kabla ya kuanza mashindano hayo ni mdogo.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Julai mjini Dar es Salaam- wakati Simba SC imepanga kuanza kambi yake ya maandalizi ya msimu mpya wiki ya kwanza ya mwezi huo.
Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba hadi sasa hawajapewa taarifa yoyote na wenyeji wa mashindano hayo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya kushiriki.
Rais wa Simba Sc, Evans Aveva amesema timu haitashiriki Kombe la Kagame

“Mwanzoni tulijaribu kuulizia ulizia kupitia watu ambao wapo TFF kama tutashiriki au la, lakini majibu yakawa si mazuri. Tulisikia kwamba, ndugu zetu Yanga walitishia kwamba sisi tukishiriki, wao watajitoa kwa sababu sisi hatustahili,”amesema Aveva.
Rais huyo amesema pamoja na kwamba dhana hiyo ya Yanga SC si sahihi kwa sababu Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) wana uwezo wa kuialika timu yoyote kushiriki mashindano hayo bila kujali nafasi yao katika Ligi ya nchi yake.
Aveva amesema pamoja na hayo TFF imeshindwa kuihakikishia Simba SC ushiriki wao kwenye Kombe la Kagame tangu wathibitishe kuwa wenyeji wa michuano ya mwaka huu na wao wameona hawawezi kufikiria kitu ambacho hawafikiriwi.
“Unadhani tungefanya nini, kuendelea kufikiria kitu ambacho hatufikiriwi ni kupoteza muda ambao kumbe tungeutumia kufanya mambo mengine kwa ustawi wa klabu yetu,”amesema Aveva.
Ameongeza kwamba, hata wakipata mwaliko kuanzia sasa ni vigumu kuukubali kwa sababu muda uliobaki kabla ya kuanza mashindano ni mdogo.
“Tunategemea mwalimu wetu mpya atafika hapa mwanzoni mwa Julai ndiyo tuanze maandalizi ya msimu mpya. Na hatutarajii kuwa na wachezaji wote, kwa sababu wachezaji wetu zaidi ya 10 wapo timu za taifa. Tutakuwa na wachezaji kama 13 mazoezini, tutashiriki vipi Kombe la Kagame,?” amehoji Aveva.
Rais huyo wa Wekundu wa Msimbazi ameongeza kwamba hata kitaalamu si vyema kuingiza timu kwenye mashindano kabla wachezaji hawajawa fiti ipasavyo.
Wachezaji wa Simba SC wakisherehekea baada ya kutwaa Kombe la Kagame mwaka 1991 mjini Dar es Salaam

“Wachezaji wetu ambao hawako timu za taifa wamekuwa mapumzikoni tangu mwezi uliopita baada ya kumaliza Ligi Kuu. Sasa hawa watu huwezi kuwaita mazoezini baada ya wiki moja uwaingize kwenye mashindano. Ni hatari, anaweza kuumia mtu ukamkosa mwaka mzima,”amesema.
Avema amesema ‘kiroho safi’ kabisa wanazitakia kila la heri timu nyingine za Tanzania zitakazoiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo.
Simba SC ndiye bingwa mara nyingi zaidi wa Kombe la Kagame, mara sita ikiwa imetwaa taji hilo katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, wakati wapinzani wao, Yanga SC wametwaa mara tano katika miaka ya 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012 sawa na Gor Mahia, katika miaka ya 1976, 1977, 1980, 1981 na 1985 na Tusker zote za Kenya miaka ya 1988, 1989, 2000, 2001 na 2008.
APR ya Rwanda imetwaa mara tatu 2004, 2007 na 2010 sawa na El Merreikh ya Sudan 1986, 1994 na 2014 na SC Villa Villa ya Uganda katika miaka ya 1987, 2003 na 2005.
KCC ya Uganda, Atracao, Polisi na Rayon za Rwanda na Vital’O ya Burundi kila moja imetwaa mara moja moja taji hilo.
Kwa mujibu wa kanuni, bingwa na mshindi wa pili hadi wa tatu mara nyingine kwa nchi mwenyeji hupata nafasi ya kucheza mashindano hayo, wakati nchi nyingine hutoa timu moja. Nchi ambayo ilitoa bingwa wa mashindano yaliyopita hupeleka timu mbili.
Lakini CECAFA, imekuwa ikialika timu yoyote iitakayo kucheza ili kunogesha mashindano kulingana na mvuto wake kwa mashabiki- mara nyingine hualika hadi klabu za nje ya ukanda huu. 
Ilitarajiwa Simba SC, ambao ni wapinzani wa jadi wa Yanga SC, timu zenye mashabiki wengi zaidi ukanda wote huu, ingeshiriki pia mashindano hayo, ingawa msimu uliopita ilimaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu nyuma ya Azam FC, Yanga SC na Mbeya City.
Msimu huu uliomalizika Mei, Simba SC ilimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Yanga SC na Azam FC na mwakani iwapo Tanzania itaandaa tena mashindano hayo, basi watakuwa na fursa ya kushiriki kwa mujibu wa kanuni ‘bila kubembelezwa’.
Lakini mashindano yakienda nje ya Tanzania, ni Yanga SC peke yao watakaosafiri.