Monday, June 8, 2015

SOMA BARUA HII NZITO ALIYOAANDIKIWA DIAMOND PLATINUMZ NA MMOJAWAPO WA WAFUASI WAKE

diamond platnumz

KWAKO supastaa usiye na mpinzani Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond’, habari za siku kaka? Pole kwa mishemishe na harakati za muziki wako.Ukitaka kujua hali yangu, mimi ni mzima wa afya. Namshukuru Mungu kwa kunijalia uzima, naendelea kupambana na maisha kama kawa.
Dhumuni la barua hii kwanza ni kutaka kuzungumza na wewe kuhusiana na suala zima la kuwasomesha watoto ambao mwaka jana uliahidi kuwalipia ada katika Shule ya East Africa International jijini Dar.Kwanza nikupongeze kwa wazo lile. Lilikuwa zuri mno, hakuna muungwana yeyote anayeweza kubeza wazo hilo hata kidogo. Binafsi nilifurahi kwani nilijua umetambua umuhimu wa kurudisha fadhila kwa jamii.
Ulionesha  moyo wa upendo. Ni wachache sana ambao wanaweza kuwa na moyo wa aina hiyo. Wapo matajiri wengi tu wenye fedha kama zako au zaidi lakini hawakuguswa kufanya hivyo, wewe uliona umuhimu huo ukaamua kwenda kuwasaidia. Pongezi kwako.
Pamoja na pongezi zangu, nina neno kidogo. Niliposoma habari ya wewe kushindwa kuwalipia ada wiki iliyopita, nilishtuka. Kwamba ni kweli umeamua kuwatelekeza?
Nilienda mbali zaidi kimawazo, nikajiuliza kwamba ni wewe kweli au watu wako wa karibu ndiyo walikuangusha. Nikajiuliza au pengine ni majukumu ya shoo za nje ya nchi ndiyo yamesababisha ushindwe kuwalipia? Sikupata jibu la moja lakini nilipata shaka na majibu ya mameneja wako, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ na Said Fella.
Walionesha kwamba walikuwa na majibu ya ‘danadana’ kwa wazazi wa watoto wale ulioahidi kuwasomesha. Majibu yale yana maana mbili, moja unayaafiki au huyaafiki.Kama uliwapa jukumu la kulipia fedha hizo kwa nini hawakufanya hivyo? Kama pia jukumu lilikuwa la kwako mwenyewe kwa nini ulikaa kimya hadi kufikia hatua ya kutimuliwa shule?
Naamini wewe ni muungwana, baada ya habari ile kuchapishwa gazetini wiki iliyopita, naamini utakuwa umeshapata jibu la wapi uliteleza hadi watoto hao wakapatwa na janga hilo.Nafasi bado unayo, naamini kabisa hadi kufikia hatua ya kuamua kuwasomesha shule ile ya gharama, ulishajua uwezo unao na ndiyo maana ulithubutu kuwasomesha.
Ili kulinda heshima na hadhi yako katika jamii, chondechonde fanya kila linalowezekana wale watoto warudi shule ili na wao waje wajivunie elimu waliyoipata kutokana na mfuko wako.
Huwezi jua kati ya watoto hao watapatikana viongozi wakubwa katika nchi hii ambao wataweza kusaidia wengine. Dunia ya leo inatupasa kusaidiana. Wewe umewezeshwa kitu fulani basi ni vyema ukamuwezesha na mwingine ili aweze kutimiza ndoto zake.
Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na utalifanyia kazi jambo hili na Mungu akupe nguvu uweze kulifanikisha.
Kila lakheri, mimi ni swahiba wako