Friday, July 10, 2015

FAHAMU Kuhusu Mkoa Mpya na Wilaya SITA Mpya Zilizoanzishwa na Serikali ya Tanzania!

Serikali imetangaza kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Songwe na wilaya mpya sita zikiwemo Ubungo, Kigamboni na Tanganyika. Mkoa wa Songwe ulikuwa sehemu ya Mkoa wa Mbeya. 

Licha ya Ubungo na Kigamboni za Dar es Salaam, Tanganyika ya Kigoma, wilaya nyingine zilizoanzishwa ni Kibiti mkoani Pwani, Songwe mkoani Songwe na Malinyi mkoani Morogoro . 

Akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 20 wa Bunge jana mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema ugawaji wa maeneo hayo unafanyika kila baada ya muda kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo ongezeko la idadi ya watu na pia kuharahisisha utendaji wa serikali. 

Kuongezwa kwa Mkoa wa Songwe kunafanya idadi ya mikoa ya Tanzania Bara kufikia 26.Mikoa mingine iliyoongezwa katika Serikali ya Awamu ya Nne ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. 

Awali, mikoa ya Tanzania Bara ilikuwa 21, ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.

Zanzibar ipo mikoa mitano, ambayo ni Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Mkoa wa Mjini, Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

Waziri Mkuu alisema pia Serikali imepandisha hadhi Halmashauri za Wilaya Malinyi, Buchosa, Madaba, Manyoni, Mpimbwe, Nsimbo, Mlale, Itilima, Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kyerwa, Chemba, Mbogwe, Nyang’wale, Butiama, Mkarama, Kaliua, Bumbuli na Msalala. 

Alizitaja halmashauri za miji na Manispaa zilizoanzishwa ni Chalinze, Ifakara, Newala, Kondoa Mafinga, Nanyumbu, Mbulu, Mbinga, Bunda, Tunduma, Nzega, Handeni, Kasulu, Geita, Masasi, Ilemela, Kahama na Nzega. 

Pia alisema kuna tarafa mpya tano ambazo ni Mchemwa iliyopo Newala, Mchichila, Mangombwa, Mambamba na Mangombya, zote zipo Tandahimba. Pia kuna kata mpya 586 zimeanzishwa sehemu mbalimbali nchini. 

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, yapo maeneo ambayo ni chini ya utawala wa Rais moja kwa moja na yapo ambayo yapo chini ya mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa. 

Pia alizungumzia uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura na kusema kuwa unaendelea vizuri na uchaguzi utafanyika Oktoba 25 kama ilivyopangwa. 

Alisema uandikishaji unaenda vizuri na kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeshaandikisha watu milioni 11.2, kati ya watu milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa. Mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar uandikishaji haujaanza. 
Alisema uchaguzi utakuwa huru na wa haki, amani na utulivu, hivyo wananchi wajiandae kuchagua viongozi watakaoona wanafaa.