Friday, July 10, 2015

KUMEKUCHA! MGOMBEA URAIS UKAWA KUJULIKANA KESHO

Baada ya vikao mfululizo wiki hii, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)unatarajia kumtangaza mgombea urais wake kesho. 

Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada ya kikao cha viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD, Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi kilichofanyika juzi, mambo kadhaa yameafikiwa na kama hakutokuwa na mabadiliko yoyote, mteule wa urais kupitia umoja huo atabainishwa.  

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alithibitisha kuwa tayari makubaliano ya kugawana kata na majimbo kwa nafasi za udiwani na ubunge yamekamilika na kilichobaki ni utekelezaji.

“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” Dk Makaidi. 

Siku chache baada ya baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda, Jumanne ya wiki hii Chadema ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo kadhaa ya kitaifa.  

Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi wa waandamizi wa Ukawa walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja huo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.  

Hata baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema iliendelea na vikao vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha jina la mgombea urais.  

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alithibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani vya chama hicho na kueleza kuwa hawezi kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na kwamba kesho taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.