Thursday, July 2, 2015

Tume Ya Uchaguzi Yatangaza Kuanza Uandikishaji BVR Dar es Salaam na Pwani


Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) lililoahirishwa katika jiji la Dar es salaam na mkoa wa Pwani hivi karibuni sasa litafanyika kuanzia  Julai 7-20 kwa mkoa wa Pwani na Julai 16- 25 kwa jiji la Dar es salaam. 

Uboreshaji wa Daftari hilo kwa jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani uliahirishwa kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya uboreshaji kutoka mikoani ambavyo vilipelekwa ili kuongeza ufanisi kutokana na maeneo hayo kuwa na idadi kubwa ya watu wenye sifa ya kuandikishwa kuwa Wapiga Kura.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Mallaba amewataka wananchi wote wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya uandikishaji vitakavyokuwa kwenye Vijiji, Vitongoji na Mitaa ili kujiandikisha  waweze kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba Mwaka huu.

Amewataja watakaohusika na zoezi hili kuwa ni watu wote waliotimiza umri wa Miaka 18 na kuendelea na wale watakaotimiza Miaka 18 ifikapo mwezi Oktoba Mwaka huu.

Wengine ni waliojiandikisha awali kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la zamani ili kuhuisha taarifa zao na kupata kadi mpya za kupigia kura. Aidha Mallaba amewataja wengine wenye sifa ya kujiandikisha kuwa ni wale wote wenye sifa za kujiandikisha lakini hawajawahi kujiandikisha kwenye Daftari hilo.

Amesema wale wote wenye Kadi za kupigia Kura za zamani wanatakiwa kwenda na Kadi zao ili kurahisisha uchukuaji wa taarifa zao na kadi hizo zitarudishwa NEC na watapata vitambulisho vipya.  Wananchi wanatakiwa kujiandikisha katika Vituo vilivyopo ndani ya Kata zao ili kuweza kupata fursa ya kumchagua Diwani, Mbunge na Rais.

Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa wananchi wa mikoa hiyo kuhakikisha wanajiandikisha kwani bila kufanya hivyo hawataweza kupiga Kura wakati wa Uchaguzi Mkuu. Vituo vya kujiandikisha vitafunguliwa kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa ifikapo saa 12:00 jioni.