Vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana vimeshindwa kumtangaza mgombea urais kama ambavyo ilikuwa imetangazwa hapo awali huku wakiahidi mgombea huyo kujulikana ndani ya siku ya siku saba.
Aidha, Jana kulikuwepo na kikao cha vyama vinavyounda ukawa kilichofanyika kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam, lakini baadhi ya wafuasi wa Ukawa akiwemo Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na naibu wake wa Bara, Magdalena Sakaya walisusia kikao hicho suala linalozua maswali mengi kwa wafuasi wa vyama hivyo pamoja na wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia amesema kwamba mazungumzo yamekamilika na mgombea urais wa Ukawa atajulikana ndani ya siku saba huku akisisitiza kuwa hakuna mpasuko ndani ya umoja huo.
Inadaiwa kuwa hoja kubwa ilikuwa katika suala la mgombea urais, nafasi ambayo inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye aliyechukua fomu kupitia CUF na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye anakubalika na kuungwa mkono na vyama vyote vinne.
Kwa upande mwingine kutohudhuria kikao hicho kwa viongozi wa CUF kunaweka giza nene mbele ya vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD
Hata hivyo, kumekuwa na tetesi katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba Mbunge wa Monduli Edward Lowassa ana mpango wa kutimkia upinzani mara baada ya jina lake kukatwa CCM, hata hivyo Lowassa hajaweza kuzungumzia suala hilo na kuahidi kuandaa mkutano na waandishi wa Habari kwa lengo la kutangaza mipango yake katika siasa.