TIMBWILI! Njemba mmoja mkazi wa Kisimani mjini Tunduma wilayani Momba, Mbeya ambaye jina lake halikupatikana mara moja, amejikuta akila kichapo kisa, kudaiwa kumtorosha msichana wa kazi ‘hausigeli’ wa mtu.
Tukio hilo lililokusanya watu kibao, lilijiri juzikati katika maeneo hayo baada ya vijana hao kumtuhumu kijana huyo kwamba amemficha msichana huyo ambaye bosi wake aitwaye Johnson alikuwa akimtafuta.
Wakizungumza na Amani kuhusu tukio hilo, mashuhuda walisema vijana hao walipofika kwa mtuhumiwa huyo walimtaka aoneshe alipo hausigeli huyo ambaye ilisadikiwa kuwa yeye ndiye alikuwa naye.
“Wale vijana walisema walipeleleza na kubaini kwamba, msichana huyo wa kazi yupo naye kwa sababu amekuwa akionekana naye mara kwa mara na kuna watu wanaamini kwamba anatokanaye kimapenzi.
“Mtuhumiwa aliposema hajui alipo msichana huyo ukatokea ugomvi mkubwa, wakimshika ili wampeleke Kituo cha Polisi Tunduma lakini walitokea watu wenye kutaka amani wakamtorosha mlalamikiwa huyo kwenda kumficha mahali kusikojulikana,” kilisema chanzo.
Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Lupasyo Kingdom aliyedai anazijua sheria ya Tanzania, alisema: “Kwa utaratibu wa sheria ilibidi wao waende polisi kutoa taarifa za kupotelewa na msichana wa kazi halafu polisi ndiyo waanze kumtafuta na si wao kuchukua jukumu la kutaka kumburuza polisi mtu wanayedhani anahusika.”