Thursday, August 13, 2015

MRISHO MPOTO: AZALIWA NA MAAJABU SHINGONI, ATAKIWA KUFUKIWA

MPENZI msomaji, baada ya wiki iliyopita kumalizika kwa simulizi tamu yenye kukufunza mambo mengi ya kiroho kutoka kwa Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) lenye makao yake makuu Ubungo-Kibangu jijini Dar, Lusekelo Anthony ‘Mzee wa Upako’, wiki hii tunawaletea simulizi nyingine mpya.
Simulizi hii inamhusu mwandishi wa vitabu vya mashairi na hadithi zenye mafunzo, msanii wa ngoma za asili nchini Tanzania, Mrisho Mpoto ambaye anafahamika zaidi kwa jina la Mjomba. UNGANA NAYE...
(Anaanza kwa kujiweka sawa na kunyanyua mikono kwa ishara...)
“Kwanza kabisa nimezaliwa Oktoba 27, mwaka 1978 na kuitwa jina la Mrisho Issa Hussein Mpoto.
Mimi ni mwenyeji wa Songea mkoani Ruvuma nikiwa mtoto wa 36 kati ya watoto 36 wa Mzee Issa Hussein Mpoto. Mama yangu Mwanaisha Athumani ni mke wa mwisho wa Mzee Mpoto, yaani mke wa 12 kati ya wake 12,” anaanza kusimulia Mpoto.
Dah! Imenishtua kidogo. Namuuliza kuhusu mama yake anipe historia japo kwa ufupi, anajiweka sawa kisha ananijibu:
“Mama yangu alikuwa amejifungua watoto 12 na mimi nilikuwa wa 12 kwake. Kwa upande wa mzee Mpoto yeye ni mwenyeji wa Songea, Ruvuma, wakati mama yangu ni mwenyeji wa mkoani Pwani, sehemu moja hivi inaitwa Ikwiriri.”
Vipi kuhusu historia yake baada ya kuzaliwa? Mpoto anafunguka:
“Nimekulia na kuzaliwa Songea. Katika historia ambayo sitaweza kuisahau maishani mwangu ni kwamba, mama yangu, watoto wake walikuwa wakifariki dunia sana kutoka 12 hadi kufikia watatu tu ambao ni kaka yangu Mashaka, dada yangu alikuwa akiitwa Bure na mimi Mpoto.”
Ananishtua kwa mara nyingine, namuuliza tena ilikuwaje dada na kaka wakaitwa majina hayo ya kushtua hivyo, anafunguka:
“Kutokana na hali aliyokuwa nayo mama yangu ya kila akijifungua mtoto anafariki dunia, alipozaliwa kaka yangu, baba alipendekeza aitwe Mashaka likiwa na maana kwa mama kuwa asiwe na mashaka atakua tu na atazaliwa mwingine hatakufa, akazaliwa mwingine, akafariki dunia. Mama akaja tena akazaa mwingine ambaye ni dada yangu, akamwita Bure ikiwa na maana kuwa kila atakayezaa ni bure tu na baada ya hapo nikazaliwa mimi, nikapewa jina (siyo la Mrisho) nitawaambia hapo mbeleni mwa hii simulizi.
“Hilo jina kwa jinsi nilivyokuwa nimepewa lilikuwa lina maana kiimani, kwani nilivyopewa tu nilikuwa naumwa sana, ugonjwa fulani ambapo ukiangalia...(ananionesha eneo la koo katika shingo yake...)
“Unaona kama kuna kovu hapa, hii walivyonieleza wazazi wangu, yaani kila nilipokuwa nakunywa maji yalikuwa yanaonekana kama yanapita, yaani kama panavimba, kifupi nilikuwa naonekana kama mtu anayetakiwa kufariki dunia wakati wowote.”
Dah! Hatari, sasa baada ya hapo ikawaje, namchokonoa ili afunguke zaidi kuhusiana na hili, anaonekana kama kuruka eneo hili lakini karatasi na kalamu niliyokuwa nayo inamshawishi, ananielewa na kuendelea:
“Kwa sababu upande wa baba alikuwa na watoto wengi, akamwambia mama inabidi anipeleke nikakae naye porini hadi nitakapofariki dunia, anifukie hukohuko kisha arudi kwa sasabu kufa ilikuwa ni kitu cha kawaida.”


Simulizi hii ndiyo kwanza inaanza, je, Mrisho atapelekwa porini? Itakuwaje? Tukutane wiki ijayo