Tuesday, September 8, 2015

MIRATHI NUSURA IMTOE ROHO!

Masanga Said Bori, anayevuja damu.
Boniphace Ngumije na Mayasa Mariwata
BALAA! Mkazi wa Mtaa wa Manyoni, Ilala jijini Dar aliyejulikana kwa jina la Masanga Said Bori (pichani), Jumamosi iliyopita nusura atolewe uhai akitetea mirathi ya nyumba iliyoachwa na shangazi yake, Mwanafatima binti Mchinga akiwa na ndugu zake, Panya Bori, Mchinga Bori, Mwanafatima Bori na Zaujiha Bori.
Kwa mujibu wa chanzo, nyumba hiyo namba 27/1 yenye mirathi namba 79/2006 waliyorithishwa ndugu hao na shangazi yao ambaye ni marehemu, alipewa kusimamia mzee mmoja aitwaye Said Athuman Kingo akiwa ni mmoja wa familia hiyo.
“Muda mfupi tangu shangazi yao afariki dunia, Masanga alionekana kutoelewana na ndugu zake kwa sababu alikuwa anapangisha baadhi ya vyumba bila kuwashirikisha jambo lililowafanya wafikishane Mahakama ya Mwanzo Ilala ambapo baada ya shauri lao kusikilizwa, iliamriwa nyumba hiyo iuzwe ili wagawane pesa.
Sintofahamu ikiendelea eneo la tukio.
“Wakatafuta mteja, wakampata kwa shilingi milioni mia moja, Masanga akakataa nyumba hiyo kuuzwa kwa kiasi hicho akidai thamani yake ni kubwa, akataka iuzwe kwa shilingi milioni 160. Mahakama ikampa yeye muda wa wiki tatu kutafuta mteja lakini hakuweza kumpata,” kilisema chanzo.
...Wakiamuliwa.
Kikaendelea: “Masanga alipomkosa mteja baada ya muda huo kupita mahakama ilitoa ridhaa ya nyumba kuuzwa kwa kiasi cha shilingi milioni 100, jambo lililofanyika na baada ya hapo warithi wakagawana shilingi milioni 24 kila mmoja huku pesa za Masanga zikienda kuhifadhiwa kwenye mfuko wa hifadhi wa mahakama.
Maofisa wa Jeshi la Polisi wakifika eneo la tukio kutuliza ghasia.
“Masanga hakwenda kuchukua pesa zake badala yake akarudi mahakamani na kutaka shauri hilo libadilishwe lakini haikuwezekana. Mahakama ikatoa ridhaa kwa wanunuzi wa nyumba hiyo, Zulfa Jumanne Ileswa na Mwajuma Jumanne Ileswa wamtoe kwa nguvu kwa kutumia Kampuni ya Madalali ya Rimina ambao walikwenda kuifanya kazi hiyo sanjari na kuibomoa.
“Lakini baada ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kufika kwenye nyumba hiyo, Masanga hakukubali nyumba ibomolewe jambo lililozua timbwili zito na mtaa kufungwa kwa wingi wa watu na fujo.
“Huwezi amini, Masanga  alitoka ndani na panga kupambana na wafanyakazi wa Rimina lakini ile anataka kumkata baunsa wa kampuni hiyo, alikwepa na kumnyang’anya  kisha kumkata nalo yeye kichwani. Damu zilianza kumwagika chapachapa.”
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, baada ya hapo hali ya amani ilivurugika jambo lililofanya wasamaria wema kutoa taarifa Kituo cha Polisi, Ilala ambapo askari walifika na kutokana na vurugu zilizokuwepo walipiga mabomu ya machozi na kuzuia nyumba hiyo kuendelea kuvunjwa.
Wakamchukua Masanga na wafanyakazi wa Kampuni ya Rimina na kwenda nao kituoni kwa ajili ya mahojiano zaidi juu ya kilichokuwa kinaendelea.