Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetoa ufafanuzi kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme linaloendelea nchini linatokana na kuongeza taratibu megawati hadi zifikie megawati 335.
Meneja Mahusiano Adrian Severin alipokuwa kwenye uzinduzi wa usambazaji wa waya za umeme kwenye shule ya Msingi ya Msasani B,amesema tatizo la kukatika kwa umeme litaisha Oktoba mwaka huu baada ya bomba la gesi kujaa baa 52.
Severin amesema Septemba 19 mwa huu Tanesco iliwasha mitambo ya Umeme wa gesi asilia megawati 90 huku wakiendelea kuongeza kidogokidogo kufikia 335 ambazo zinatakiwa kutokana na ukubwa wa bomba hilo.
“Tatizo hili la kukatika kwa umeme litakuwa kwenye mikoa ambayo Gridi ya taifa imepita hivyo tulianza kuzalisha megawati 90 na tunaendelea kupandisha kiwango taratibu ili kufikia megawati 335 mwishoni mwa Oktoba mwaka huu,”amesema Severn.
Amesema Tanesco wanaendelea kuongeza kupandisha kiwango taratibu za megawati ili tatizo la kukatika kwa umeme lipungue kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Wakati huohuo Shirika hilo limesambaza nyaya za umeme zenye thamani ya Sh10 milioni kwenye vyumba 18 vya shule ya Msingi Msasani B.
Severin amesema Tanesco linajihusisha na jamii kwa kusaidia kutoa misaada mbalimbali ya maendeleo ikiwemo huduma za afya na kugawa madawati katika shule mbalimbali.
Aidha, Afisa Takwimu Geogre Maiga amesema msaada huo wa umeme utaisaidia shule hiyo kusoma kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa kutumia komputa.
“Kama umeme umeingia kwenye shule hii ninaamini kuwa ndio mwanzo wa kupata komputa ambapo wanafunzi wetu wataweza kujifunza somo la Tehama kwa vitendo,”amesema Maiga.