Pamoja na wenyewe kudai hawajui kilichotokea, mastaa wawili wenye sura za mauzo kunako sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Wema Isaac Sepetu, kwa sasa wanadaiwa kufikia pabaya kufuatia bifu zito linalofukuta kati yao.
Habari za mjini zinadai kwamba, Wema amekuwa akishtushwa na kuchukizwa na kitendo cha Lulu kuwa upande wa aliyewahi kuwa mwandani wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kiasi cha kwenda nyumbani kwake, Madale-Tegeta jijini Dar, usiku wa manane na kujiachia na jamaa huyo anavyotaka.
“Kama mtakumbuka, kabla ya kifo cha Kanumba (Steven), Wema na Lulu walikuwa ni mashosti kama ilivyokuwa kwa Wema na Snura (Mushi) au Wema na Kajala (Masanja) au Wema na Aunt (Ezekiel).
“Lakini baada ya jamaa (Kanumba) kuondoka na kisa kizima cha Lulu ndipo Wema akavunja urafiki na Lulu kwa sababu Kanumba aliwahi kuwa ‘mtu’ wa Wema kama ilivyo kwa Diamond.
“Ulipita ukimya wa muda mrefu bila Wema na Lulu kuwa mashosti zaidi ya salamu.
“Lakini mambo yalianza tena kuwa mabaya baada ya Lulu kumponda Wema alipokuwa akigombea Ubunge wa Viti Maalum kupitia CCM (Chama Cha Mapinduzi).
“Sasa hivi ishu ni kitendo cha Lulu kujiachia na Diamond kwenye birthday ya Rome Jones (binamu na DJ wa Diamond) kisha ile pati ya birthday Diamond kuifanyia nyumbani kwake huku (Lulu) akitupia picha za mafumbo yaliyoelekezwa kwa Wema.
“Hicho ndicho kinachoendelea na unaambiwa hali ni tete mno,” kilisema chanzo hicho ambacho ni mtu wa karibu wa mastaa hao.
Baada ya kupata ‘ubuyu’ kamili, Amani lilimtafuta Wema na kummwagia data ambapo alionesha kushtushwa na kudai kwamba hata yeye anashangaa ni nini kimetokea.
Kwa upande wake Lulu hakupatikana hewani lakini kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya hivi karibuni juu ya uhusiano wake na Wema, mwanadada huyo alikiri kuwa rafiki wa Wema kitambo hicho lakini akasema hajui ni nini kilichotokea zaidi ya kwamba huwa wanasalimiana tu wanapokutana.
Kabla ya mambo kwenda mrama, Lulu na Wema walikuwa mashosti wakubwa ambapo gazeti hili liliwahi kuwashuhudia wakiwa lokeshi na kulala pamoja chumba kimoja kama mtu na dada au mtu na mdogo wake.