Friday, October 16, 2015

LOWASSA Atoa Onyo Kwa Tume Ya Taifa Ya Uchaguzi.....Asema NEC Isipokuwa Makini Itavuruga Amani ya Nchi. Mbowe Katoa Mwongozo Kwa Wapiga Kura


Mgomea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ameionya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwamba kama haitakuwa makini, inaweza kuvuruga uchaguzi mkuu.

Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vinne vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitoa tahadhari hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika viwanja vya Sabasaba, mjini Magu jana.

Alitoa kauli hiyo kutokana na takwimu za wapigakura zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete juzi, zikionyesha kutofautiana na takwimu za NEC.

Akizungumza katika kilele cha mbio za mwenge mjini Dodoma juzi, Rais Kikwete alisema Watanzania waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Tanzania Bara ni milioni 28 na Zanzibar ni zaidi ya 500,000.

Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo ambayo baadaye ilisahihishwa na mwandishi wake msaidizi, Premi Kibanga, takwimu za NEC zinaonyesha waliojiandikisha Tanzania Bara ni milioni 22.7 naZanzibar ni 503,193.

Lowassa katika maelezo yake kwenye mkutano huo wa kampeni, alionyesha kutoridhishwa na kauli ya Rais Kikwete kwa kile alichosema inatia shaka kutokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini.

“Jana (juzi) Rais Kikwete alitoa kauli kuhusu idadi ya wapigakura, lakini baadaye kauli hiyo ikabadilishwa na kukanushwa kwa sababu ilikuwa ikitofautiana na na ile ya NEC.

“Katika hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina kazi kubwa, wasipoangalia watavuruga, na uchaguzi ukivurugwa ni mwanzo wa matatizo katika nchi.

“Mimi sielewi, rais wa nchi anapewaje takwimu alafu baada ya saa mbili zinakanushwa. Huyo anayempa rais wa nchi matakwimu ya namna hiyo ni nani? Tulisema tume ni huru je, ni huru kwa hali hii ikiwa inangojea taarifa ambazo zinatofautiana na za rais?

“Nataka kutoa tahadhari na kuwaomba wawe makini, wasituharibie uchaguzi, wasituharibie nchi yetu, dhamana ya amani na utulivu juu ya mambo haya iko juu yao, nawasihi sana wawe makini wasituharibie nchi,” alisisitiza Lowassa.

Pamoja na suala hilo, Lowassa alizidi kuzungumzia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini na kusema hilo ni sawa na bomu.

“Mtu amesoma vizuri, anakaa nyumbani, kunakucha leo, kunakucha kesho, na kila siku hivyo hivyo, haiwezekani, atafanya lolote.

“Katika kukabiliana na hali hiyo, alisema Serikali yake itaboresha kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa ili kiweze kuajiri watu wengi,” alisema.

Alisema sera ya kufuta kodi zote kwenye mazao ya chakula, inalenga kuhakikisha mkulima anafaidika na kilimo.

Njia ya pili aliyosema ataitumia kutoa ajira kwa Watanzania, ni kuhakikisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaongezewa uwezo mara tano zaidi ya lilivyo sasa, ili pamoja na mambo mengine, litoe zaidi mafunzo ya ufundi na stadi zitakazowawesha vijana kujiajiri.

Mbowe atoa elimu mpya kwa wapigakura
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, akizungumza na wananchi hao, alitoa elimu kwa wapigakura, aliyosema inalenga kuokoa kura ambazo zinaweza kuharibika.

“Ukishapiga kura yako, ukunje karatasi wakati picha za wagombea zikiwa zinaangalia nje, tofauti na ilivyozoeleka ambapo karatasi hukunjwa picha na majina ya wagombea yakiwa ndani. Lengo la kukunja kura picha za wagombea zikiwa nje ni kuepuka kura za maruhani ambazo zitaharibika.

“Nawashauri pia wote mnaoweza kubeba kalamu zenu na kwenda nazo vituoni, mwende nazo wala msiziamini zile za NEC. Mkishapiga kura kaeni mita 200 ili kuzilinda.

“Wanasema tukipiga kura tukalale, hapa hakuna kulala, nyumbani hatuendi, tutahesabu mita 200 tutapiga kambi mpaka matokeo yatangazwe, uchaguzi ni maisha yetu na uchaguzi wa mwaka huu ni wa mabadiliko.

“Sisi tunasema hatutaki magari yasiyohusika kuingia vituoni, mkienda kulala wataiba kura, polisi simamieni kura, msitake kuingiza taifa kwenye machafuko, sisi tutasubiri matokeo,  tutakesha hata kama yatatoka kesho yake,” alisema Mbowe.