Tuesday, October 13, 2015

MTUHUMIWA WA UGAIDI ANASWA NA POLISI JIJINI DAR


Mtuhumiwa huyo akiwa kituoni.
Na Makongoro Oging’
HALI tete! Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke, Dar lilifanikiwa kumdhibiti mtu mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja kufuatia madai ya kuvamia Kituo cha Polisi Charambe akiwa na panga.
Habari zilizopatikana kutoka kwa raia wa eneo hilo ambao walimtafsiri mtu huyo kama gaidi kutokana na ujasiri wake wa kuvamia kituo kwa mapanga kwa lengo la kutaka kuwajeruhi askari kituoni hapo bila uoga.

Uwazi ambalo lilifika kituoni hapo mara baada ya tukio hilo, liliambiwa kwamba mtu huyo alijitokeza kituoni hapo majira ya saa sita mchana na kuanza kuwapiga polisi na ubapa wa panga hali iliyozua tafrani.
Wananchi hao kwa nyakati tofauti walisema kwamba, mtu huyo alikuwa na nguvu nyingi kiasi cha kuwafanya askari kuchukua muda mrefu kumdhibiti kwani hapa kumpiga pingu ilikuwa shughuli pevu.

Taarifa zaidi toka kwa wananchi hao zinadai kwamba, ili askari waweze kumdhibiti ilibidi afungwe pingu haraka. Hata hivyo, licha ya kujeruhiwa miguu bado alikuwa akiongea kwa sauti ya juu nje ya kituo hicho, akiwalaani askari hali iliyowafanya wananchi kuzidi kujaa huku wakidai si mtu wa kawaida.

Vyanzo vingine makini vilidai kwamba, kutokana na hali iliyojitokeza kwa mtu huyo kutotii amri ya polisi iliwafanya askari waongezeke baada ya kupigiwa simu kwa hofu kuwa huenda ana wafuasi wake ambao wangeweza kuvamia kituo wakati wowote.
Vyanzao hivyo viliendelea kudai kwamba zaidi ya difenda tatu ambazo zilikuwa na polisi zilifika kituoni hapo muda mfupi baadaye na kila askari alionekana akiwa tayari kwa lolote.
Ilidaiwa kwamba hali hiyo ilimfanya Kamanda wa Polisi Temeke, ACP Andrew Satta kufika ili kushuhudia hali hiyo kwa macho.
Baadhi ya wananchi walisema mtu huyo alikuwa na wenzake ambao haikujulikana walikoelekea na ndiyo sababu polisi walipatwa na hofu. Mtu huyo alichukuliwa hadi Kituo cha Polisi Mbagala kwa mahojiano zaidi.
Kamanda Satta alipohojiwa na Uwazi kwa njia ya simu alisema hayupo ofisini hivyo alimtaka mwandishi kufika ofisini kwake. Mwandishi alipofika hakumkuta ofisini na simu yake ilipopigwa ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Bado gazeti hili linaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu ili kujua ni kitu gani kilitokea.