Wednesday, October 14, 2015

Serikali Yakanusha Data za Mawasiliano na Umeme Kuzimwa Siku ya Uchaguzi


SERIKALI imeeleza kushangazwa na uzushi kwamba siku ya uchaguzi mkuu, data za mawasiliano pamoja na umeme vitazimwa, jambo ambalo imetaka wananchi kupuuza taarifa hizo potofu.

Taarifa hizo ambazo Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ameziita ni uzushi, zinadaiwa kutolewa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wakidai kwamba serikali imepanga kufanya hivyo ili wananchi washindwe kupata taarifa za matokeo ya uchaguzi.

“Kwanza napenda ifahamike kuwa hakuna chama chochote cha siasa kitakachofaidika kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), endapo data za mawasiliano zitazimwa, hivyo nawaomba wananchi wasiamini maneno ya uzushi yasiyo na ukweli hata chembe,” alisisitiza January.

Alisema huduma ya data zina umuhimu mkubwa katika uchumi wa Tanzania kuliko siasa, kwani kwani ofisi nyingi zikiwemo taasisi za kibenki zinategemea data hizo katika shughuli zake za kila siku.

“Sasa ukisema tutazima data ni sawa na ku-paralyze (kusimamisha) uchumi kwani watu hawataweza hata kutoa fedha zao benki, jambo ambalo ki ukweli haliwezi kufanyika,” alisisitiza.

Alisema ni Wizara yake na Serikali kwa ujumla, imekuwa ikilinda na kurekebisha mitandao kuhakikisha inafanya kazi vizuri hasa katika kipindi hicho cha uchaguzi kutokana na ukweli kuwa kutakuwa na taarifa nyingi zinazohitajika kufikia wananchi.

Hatutegemei watu kutumia vibaya mitandao ya kijamii na kusababisha taharuki lakini hata wakifanya hivyo, Sheria ya kudhibiti mitandao ipo, itatumika kudhibiti na si kuzima data kama inavyodaiwa,” alisema January.

Aidha alisema taarifa hizo zilizosambazwa ambazo hata yeye ameziona, zinasambazwa na wanasiasa wenye nia ya kutengeneza hamaki kwa wananchi jambo ambalo si sahihi. 
  
Wakati huo huo, msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Adrian Severine, alisema kwa sasa shirika hilo, haliwezi kuzungumzia jambo hilo, hadi pale wanasiasa wote wanaodai mtaani kuwa wanazo taarifa za kuzimwa umeme nchini siku ya uchaguzi watoe uthibitisho.

“Huu ni wakati wa uchaguzi, hawa wanasiasa watasema mengi tu, sasa sisi kama shirika hatuwezi kusema lolote wala kukanusha taarifa hizi mpaka hao wanaodai kuwa wana taarifa kuwa tumeamriwa tuzime umeme watuthibitishie. Siwezi kukanusha kitu ambacho hakina uthibitisho,” alisisitiza Severine.

Alisema kwa sasa shirika hilo, limeamua watu wote watakaozusha taarifa kuhusu utendaji au shughuli za shirika hilo na kuthibitika kuwa ni uongo, wataburuzwa mahakamani ili iwe fundisho. “Kuna watu tayari tumewafungulia mashitaka kwa ama kuandika au kuzungumzia taarifa za uongo kuhusu Tanesco, kesi zinaendelea mahakamani,” alisema.

Juzi katika mkutano wa viongozi wa siasa ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alidai kuwa chama hicho kinazo taarifa za uhakika kuwa siku ya uchaguzi umeme na data vitazimwa ili wananchi washindwe kupata taarifa za uchaguzi. Pamoja na kiongozi huyo, kutoa kauli hiyo, pia baadhi ya mitandao nayo imekuwa ikisambaza taarifa hizo.