Wednesday, November 4, 2015

CCM yampitisha mtoto wa Kigoda kugombea ubunge Handeni Mjini


Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Handeni Mjini wamempigia kura na kumchagua tena mgombea ambae alishinda awali Omari Abdallah Kigoda katika uchaguzi uliofanyika wilayani humo leo baada ya kamati kuu ya CCM Taifa kutaka urudiwe.

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti  aliyesimamia uchaguzi huo Dk Maua Daftari alisema kuwa wajumbe wote kwenye mkutano walikuwa 690 na waliopiga kura ni 660 na uchaguzi ulikuwa wa wazi na haki na hakukuwa na tatizo lolote.

Alisema Omari Kigoda amepata kura 402 na mgombea mwenzake Hamisi Mnondwa alipata kura 257 huku kura moja ikiharibika na kufanya jumla ya kura zote kuwa ni 660 hivyo kumtangaza Omari kuwa mshindi katika kura halali 259.

Awali kabla ya uchaguzi huo mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Taifa Abdallah Bulembo alisema kuwa sababu kubwa ya kurudiwa uchaguzi huo ni kutokana na mshindi wa kwanza na aliyemfuatia kushindwa kuvuka nusu ya idadi ya wapiga kura hivyo hawakufika katika vigezo vinavyotakiwa.

Mgombea huyo anatarajiwa kwenda kuchukua fomu ya kugombea ubunge kwa msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la Handeni Mjini kesho na kuirudisha ambapo tarehe tano wataanza kampeni rasmi.