Musa Mateja
ASANTE Mungu! Mume wa muimba Injili, Flora Mbasha, Emmanuel Mbasha ameangusha bonge la pati nyumbani kwake Tabata Kimanga Mwisho, jijini Dar, Jumapili iliyopita kama shukrani kwa Mungu kwa kumfanikisha kushinda kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake siku ya tukio, Mbasha alisema kwamba anamshukuru sana Mungu kwani katika kipindi ambacho kesi hiyo ilivyokuwa mahakamani, hakuwa na furaha na muda wote alikuwa akimuomba Mungu aweze kumnusuru na kifungo.
Mbasha ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya kumbaka shemeji yake nyumbani kwake, mwaka jana kipindi alichokuwa akiishi na mkewe, amesema kitendo cha yeye kuwa uraiani ni jambo la kumshukuru Mungu na ndiyo maana akaamua kuchinja ng’ombe kuwaalika ndugu jamaa na marafiki wale pamoja.
“Nina furaha mno, siwezi kuizungumzia furaha yangu lakini Mungu Baba wa Mbinguni ananijua ni jinsi gani nilivyofurahi moyoni mwangu kwani kipindi ambacho nilikuwa nikisimama mahakamani, niliiona kabisa milango ya jela mbele yangu,” alisema Mbasha.
Katika sherehe hiyo, waalikwa walikula hadi kusaza na kumshukuru Mbasha kwa kuiandaa.
“Tunamshukuru sana. Tumekula na kunywa hadi tumebakiza vingine, Mungu ni mwema, tunamuombea Mbasha azidi kufanikiwa katika maisha yake,” alisema mmoja wa waalikwa ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.