Boniphace Ngumije na Brighton Masalu
Taharuki! Katika hali ya kushtua, njemba mmoja mtata mwenye asili ya Kiarabu amezua tafrani kwenye Maduka ya Mlimani City yaliyopo Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar baada ya kudakwa akitalii na kupiga picha za mnato kwenye maeneo maalum bila kujulikana lengo lake.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, sekeseke hilo lilijiri kwenye maduka hayo mapema wiki hii, majira ya mchana ambapo jamaa huyo aliyekuwa na ‘mandevu mengi na marefu’ alitinga mahali hapo huku akiwa amevalia mavazi meusi tii.
Akiwa kwenye korido za maduka hayo, mtu huyo alianza shughuli ya upigaji picha aliyokuwa anaifanya kwa tahadhari kubwa kwa kutumia kifaa maalum chenye umbile la kamera za dijitali.
“Jamaa alikuwa akizunguka sehemu maalum alizopanga kuzifanyia kazi bila kuogopa sheria ambazo haziruhusu mtu kupiga picha maeneo hayo.
“Baadaye alitiliwa shaka kutokana na watu kuingiwa hofu juu yake kwani baadhi walikuwa wanamkimbia ndipo akadakwa na walinzi.
“Walinzi wa Mlimani City walipomkamata walimhoji kwa nini anapiga picha, akasema alikuwa analinganisha uzuri wa maduka hayo na huko kwao alikotoka,”alisema shuhuda.
“Ni kweli tukio hilo limetokea lakini lilikuwa ndani ya uwezo wetu wa vyombo vya usalama tulivyonavyo maana jamaa hakuchukua muda mrefu kufanya hivyo, alikamatwa na kuhojiwa. Baadaye aliamuriwa kuzifuta picha hizo kisha aliachiwa huru.”