Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu.
DAR ES SALAAM
ASKARI Polisi wa Kituo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wachuku Lotson Mwaipasi (51) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, wakati akijaribu kumsaidia binti yake aliyekuwa akitaka kuporwa dukani huko Bunju, nje kidogo ya jiji wiki iliyopita.
Inadaiwa kuwa hiyo ni mara ya pili kwa askari huyo kuvamiwa dukani kwake ndani ya muda mfupi, kwani Agosti mwaka huu, watu wanaodhaniwa kuwa wezi walifika na kutaka kupora.
Inadaiwa kuwa kabla ya mauaji hayo kutekelezwa na wenyewe kutokomea kusikojulikana, majambazi hao walivamia maduka mengine na kupora fedha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Camilius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema msako mkali unaendelea kuhakikisha wauaji hao wanatiwa mbaroni.
Alisema idara ya upelelezi itafanya kazi yake kwa haraka ili kuwanasa watu hao huku akitaka kupewa maendeleo ya msako huo kila mara.
Marehemu Mwaipasi alizikwa nyumbani kwao mkoani Mbeya Novemba 4, mwaka huu.