Na Haruni Sanchawa
TENA! Kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila (pichani) aliyefariki dunia Oktoba 4, mwaka huu kimetikisa upya baada ya naibu katibu mkuu wa chama hicho, Abdul Juma kutoa mwezi mmoja kwa polisi iwe imetoa majibu ya uchunguzi wake.
Akizungumza na gazeti hili juzi jijini Dar, katibu huyo alisema licha ya Oktoba 22, mwaka huu mke wa marehemu Mtikila, Georgia Mtikila kulalamikia mazingira ya kifo cha mumewe, polisi hawajatoa taarifa yoyote juu ya uchunguzi wao.
Alisema kifo cha Mtikila kilikuwa cha kutatanisha ndiyo maana mama Mtikila alimuomba rais aliyemaliza muda wake, Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi kwani wote waliopata ajali na kiongozi huyo, mpaka sasa hawajulikani walipo na hakuna hata mtu mmoja anayeshikiliwa.
Akaongeza: “DP ilikuwa na imani kubwa na Kikwete kwamba angeunda tume ya uchunguzi kwa vile aliyefariki dunia ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama halali cha siasa ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika nchi.
“Hata hivyo, DP na familia ya Mtikila ina imani kubwa kwamba, Rais John Pombe Magufuli ataliona hili kwa vile amepokea kijiti cha uongozi kutoka kwa Kikwete.”
Hata hivyo, aliongeza kwamba licha ya kuwa na imani na Magufuli, wanatoa mwezi mmoja, wakiona kimya watafanya kila mbinu ya kumuona kiongozi huyo mpya wa nchi ili ufumbuzi upatikane.