Saturday, March 12, 2016

Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako 'Atibua' Dili la Bilioni 4........Fedha Hizi Zilipangwa Kutafunwa Ndani ya Siku Nne


Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezuia Ulaji wa Sh bilioni 4 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya semina ya siku nne.

Akizungumza wakati akifunga mkutano mkuu wa tatu wa maofisa elimu mkoa na wilaya nchini, Profesa Ndalichako alisema amezuia mafunzo yaliyokuwa yagharimu Sh4 bilioni ambayo mtu mmoja alitengewa Sh4 milioni kwa ajili ya semina ya siku nne.

“Ina maana kila mtu alikuwa alipwe shilingi milioni moja kwa siku. Kweli hatuoni aibu kutumia fedha hizo kwa mafunzo. Watu walewale wanaokwenda kwa mafunzo yaleyale,” alisema. 

Alisema wakati hayo yote yakitendeka, wanafunzi wananyeshewa mvua kwa kukosa madarasa na wanakaa chini kwa kukosa madawati.

Profesa Ndalichako, pia alisema amegundua ufisadi katika Sh66 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule nchini.

Alisema Novemba mwaka jana, Serikali ilitoa Sh63 bilioni katika mikoa yote nchini, kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu.

Profesa Ndalichako alisema baadhi ya fedha hizo zilitolewa bila kufuata utaratibu sahihi, hivyo kufanya wengine kutofahamu kama kuna fedha kama hizo zilitolewa.

“Kuanzia Jumatatu nitapeleka orodha na kiasi cha fedha kilichopelekwa kwa Ma-RC (wakuu wa mikoa) na Ma-DC (wakuu Wilaya) nchini ili mzione. Fedha zitawatokea puani…cha mtu sumu, kama ulikula fedha hizo uhakikishe unazirejesha.”

Bila kumtaja jina, Profesa Ndalichako alisema kuna mtu alitumia Sh60 milioni kukarabati darasa moja la shule ya msingi.

“Hiyo ni ukarabati wa darasa tu la shule za msingi. Wale waliokula fedha hizo nawaambia zitawatokea puani, hatuwezi kuwavumilia,” alisema.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Maofisa Elimu wa Wilaya na Mikoa (Redeoa), Juma Kaponda alishauri walimu wa shule za msingi waimarishwe kwa maarifa na lugha ya Kingereza.

Hata hivyo, alisema ni vyema stashahada ya elimu ya msingi ifundishwe kwa Kingereza .