Thursday, April 7, 2016

Mama Amtupa Chooni Mtoto Wa Siku 3 Huko Ulowa Kahama Kisa Baba Wa Mtoto Atoi Matumizi.

Jeshi la Polisi katika kituo kidogo cha Bulugwa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga linamshikilia Aneth Marco(23) Mkazi wa kijiji cha Mbika kwa kosa la kumtupa Chooni mtoto wake wa Siku nne.

Akiongea na JIJI LETU mtendaji wa Kata ya Ulowa Thomas Masunga amesema kuwa Binti huyo alikitupa kichanga hicho usiku wa kuamkia leo majira ya saa nne usiku katika choo cha jirani wa ndugu yake alipokua amefikia.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio kichanga hicho kiligundulika saa kumi na moja alfajiri wakati mama ya nyumba hiyo alipoenda chooni kujisaidia na kukuta kichanga hicho kinalia na ndipo walipopiga kelele za kuomba msaada kwa majirani.

Walipofika majirani walibomoa choo hicho na kukitoa kichanga hicho kikiwa hai na kukikimbiza katika Zahanati ya Kijiji cha Kangeme na kupewa huduma ya kwanza.

Kufuatia msako uliofanywa na wananchi kwa kushirikiana na mtendaji wa kata walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na walipomuhoji sababu ya kukitupa kichanga hicho alisema kuwa Baba wa mtoto hatoi matumizi hivyo  maisha yamekua magumu.

Binti huyo inasemekana ametoka kata jirani ya Mbika na kwenda kukitupa kichanga hicho kata nyingine ili kukwepa watu wanaomfahamu katika kata yake wasifahamu dhamira yake.

Kwa sasa kichanga hicho kimehamishwa katika Zahanati ya kata ya Ulowa na kimepelekwa katika Kituo cha Afya cha Kata ya Mbika Ushetu na hali yake inaendelea vizuri.