Sunday, October 12, 2014

BASI AINA SCANIA NA COSTA TOYOTA YASABABISHA AJALI NA WATU WANNE KUFARIKI DUNIA MPANDA...SOMA ZAIDI

 
WATU wanne wamekufa na wengine 14 wamejeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda baada ya basi la Kampuni ya AN kugongana uso kwa uso na gari lingine. 

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo ilitokea jana nyakati za saa tisa alasiri katika eneo la Mtamba wilaya ya Mlele mkoani humo katika barabara ya Mpanda - Tabora.

Aliwataja marehemu kuwa ni Emanuel Kavisha, mkazi wa kijiji cha Kasansa Tarafa ya Mamba wilaya ya Mlele na mwingine alifahamika kwa jina moja la Mswaya, ambaye ni mkazi wa Tarafa ya Inyonga wilaya ya Mlele huku marehemu wengine wawili hawajafahamika majina yao.

Alisema ajali hiyo ilihusisha basi aina Scania mali ya Kampuni ya AN yenye namba za usajili T 502 ALG nililokuwa likitokea Tabora kuelekea Mpanda na Costa yenye namba za usajili T 970 ASJ mali ya Emoro, mkazi wa Kerema Wilaya ya Mpanda, lililokuwa likiendeshwa na Abdu Feruzi likiwa linatokea Mpanda mjini kwenda Tabora.

Aliwataja majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda kuwa ni Jafari Jackison, Leonald Patrick (26) David Linus (25), Donald Gabriel (43) Nicolas Wilaamu (25) wote wakazi wa tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele Wengine ni Christopher Kapaya , Jackson Shila (15), Joseph Chalula (16) wakazi wa Wilaya ya Nkasi, Rukwa ambapo majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda.

Kidavashari alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari hayo na dereva wa Costa alikimbia mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo na jeshi la polisi linaendelea kumsaka.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, Dk Jafari Kitambwa alisema hali ya majeruhi waliolazwa hospitalini hapo inaendelea vizuri.